Na Calvin Gwabara – Morogoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimetoa jumla ya tuzo 242 kwa washindi 205 waliobobea katika taaluma,
utafiti na uongozi, huku tuzo hizo zikitolewa kwa msaada wa wafadhili 56 katika
hafla ya 43 ya utoaji wa tuzo iliyofanyika leo katika Kampasi ya Edward
Moringe, Morogoro.
![]() |
| Baadhi ya wahitimu wakifuatilia hafla ya zoezi la utoaji wa tuzo hizo. |
Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Fabian Magawa Madele, aliwataka wanafunzi waliotunukiwa tuzo kutotazama mafanikio hayo kama mwisho wa safari yao, bali kama mwanzo wa majukumu na fursa kubwa zaidi katika maisha yao ya kitaaluma na kikazi.
Aidha amesema tuzo hizo ni
matokeo ya bidii, nidhamu, uvumilivu, utafiti na kujituma, hivyo zinapaswa
kuwahamasisha washindi kuongeza juhudi zaidi.
Dkt. Madele, ambaye aliwahi kuwa
mwanafunzi wa SUA kati ya mwaka 1995 na 2000 akisomea Shahada ya Udaktari wa
Mifugo, amesema kurejea chuoni hapo kama kiongozi wa Serikali kwake ni zaidi ya
hafla na Heshima kwakuwa SUA imekuwa msingi wa elimu na taaluma yake huku
akiwataka wahitimu na wanafunzi kutumia maarifa waliyoyapata kwa manufaa ya
jamii na Taifa, huku wakizingatia ubunifu, uadilifu na uwajibikaji.
“Kuwa
bora, kuwa wabunifu, kuwa na nidhamu, kuwa watu wa uadilifu na, zaidi ya yote,
tumieni maarifa yenu kuitumikia jamii na kujenga Taifa letu lakini
nisisitize mafanikio ya kitaaluma
yanapaswa kuambatana na matumizi ya maarifa katika kutatua changamoto za jamii
na kuchangia maendeleo ya Tanzania,”
alisema Dkt. Madele.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa
SUA, Prof. Raphael T. Chibunda, alisema tuzo 242 zilizotolewa mwaka huu
zinajumuisha tuzo 214 za taaluma, 23 za
uongozi na tano za utafiti, huku wanafunzi 45 wakifanikiwa kupata tuzo
zaidi ya moja huku tuzo 18 zimetolewa kwa washindi zaidi ya mmoja, jambo
linaloonyesha upana wa mafanikio yanayotambuliwa na Chuo hicho.
Prof. Chibunda amesema SUA
imeendelea kuweka mkazo mkubwa katika utafiti na ubunifu kama sehemu ya
utekelezaji wa dhamira yake ya kuzalisha maarifa yanayochangia maendeleo na
katika hafla hiyo watafiti watano walitambuliwa kwa kazi zao za utafiti
zilizoonyesha ubora wa kipekee na mchango katika kuongeza maarifa na maendeleo,
huku pia wanafunzi viongozi waliopatikana kupitia mchakato wa uwazi na
kidemokrasia wakitunukiwa kwa uongozi wao bora.
Aidha, Prof. Chibunda amesema
Chuo kinaendelea kutambua ubora wa kitaaluma kupitia tuzo mbalimbali, ikiwemo Tuzo
kwa wanafunzi bora yaw a Uzamili “Convocation Prize for the Best Master’s Student”
iliyoanzishwa mwaka 1989 kwa ajili ya kumtambua mwanafunzi bora wa Shahada ya
Uzamili.
Aidha amefafanua kuwa tuzo hiyo
ina vigezo vigumu, ikiwemo kuwa na wastani wa alama (GPA) wa 4.0 au zaidi,
kumaliza masomo yote SUA na kukamilisha na kuwasilisha tasnifu ndani ya miaka
miwili.
“Hafla hii ni fursa ya kutambua na kusherehekea
wanafunzi na watumishi waliojitofautisha katika ubora wa kitaaluma, uongozi na
utafiti, na pia kuhamasisha jumuiya nzima ya Chuo kufikia viwango vya juu zaidi
vya utendaji na mafanikio,” alisema Prof. Chibunda.
Amesema mafanikio hayo
yanafanyika wakati SUA ikiendelea kutekeleza mpango mkakati wa Chuo kwa lengo
la kuimarisha ushindani wake na kujenga mazingira yatakayowawezesha wanafunzi
na watumishi kutumia uwezo wao kikamilifu.
Akizungumza wakati akimkaribisha
Makamu mkuu wa Chuo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa
Kitaalamu, Prof. Maulid Mwatawala
amesema hafla hiyo hufanyika kila mwaka kabla ya mahafali kwa lengo la kutambua
wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao pamoja na watumishi walioonyesha
ubora katika taaluma, hususan kupitia tafiti zenye tija kwa jamii na taifa.
Prof. Mwatawala amesema kwa kuwa
wanafunzi na watumishi wote wanafanya vizuri katika majukumu yao lakini tuzo
hizo hutolewa kwa wale waliofanya vizuri zaidi, jambo linalolenga kuwahamasisha
wengine kuongeza juhudi katika masomo na utendaji wa kazi.
“Pamoja na upande wa taaluma
lakini pia tuzo hizi zilitolewa pia kwa
viongozi wa Serikali ya Wanafunzi (SUASO) kutokana na mchango wao katika kipindi
cha mwaka mzima wa masomo, hususan katika kuimarisha ushirikiano kati ya wanafunzi,
uongozi wa Chuo na walimu kwani viongozi hao wamekuwa kiungo muhimu katika
kufikisha na kusikiliza masuala yanayowahusu wanafunzi”Alisema Prof. Mwatawala.
Aidha amesema kuwa mafanikio ya
tukio hili la utoaji wa tuzo hayategemei Chuo pekee bali pia ushirikiano wa
taasisi, mashirika na watu binafsi wanaochangia zawadi mbalimbali kwa wanafunzi
na wanataaluma na hivyo amewashukuru wafadhili 56 waliowezesha tuzo hizo kwani
mchango wao unasaidia kujenga utamaduni wa ubora na kuwahamasisha wanafunzi na
watafiti kufanya vizuri zaidi.
Akitoa shukrani kwa mgeni rasmi
kabla ya kuhitishwa kwa tukio hilo Naibu makamu makuu wa Chuo Upande wa Utawala
Fedha na Mipango Prof. Amandus Muhairwa amemshukuru mgeni rasmi kwa kutenga
muda wake kuja kujumuika na Chuo kwenye hafla hiyo pamoja na kuwa na majukumu
mengi ya kitaifa.
Amepongeza juhudi kubwa
zilizofanywa na wanwake kwenye tuzo za mwaka huu hasa baada ya kuonekana tuzo
nyingi kuchukuliwa na wanawake na hivyo kutoa changamoto kwa viojana wa kiume
kuona namna ya kuongeza juhudi kwenye masomo yao badala ya kukaa na kuchwa
nyuma kwenye masomo.
Hafla hiyo imefanyika ikiwa ni
siku moja kabla ya Mahafali ya 48 ya SUA yanayotarajiwa kufanyika kesho, ambapo
jumla ya wanafunzi 3,309 kutoka
programu 69 wanatarajiwa kutunukiwa shahada mbalimbali.
MATUKEO KATIKA PICHA WAKATI WA ZOEZI HILO LA UTOAJI WA TUZO.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia Mifugo Dkt. Fabian Magawa Madele akizungumza kabla ya kuanza kutoa zawadi kwa wahitimu. 
Baadhi ya Viongozi wa Menejimenti ya Chuo wakifuatilia hotuba ya Mgeni rasmi wakati wa hafla ya utoaji wa zawadi kwa wahitimu na wafanyakazi.














0 Comments