Na: Calvin Gwabara - Morogoro.
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimeendelea kuimarisha nafasi yake katika elimu ya juu, utafiti na
ubunifu, huku kikizindua hatua mbalimbali za kimkakati zinazolenga kuongeza
mchango wa Chuo katika maendeleo ya Taifa.
| Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Mhe. Jaji Mkuu mstaafu Joseph Sinde Warioba akimtunuku mmoja wa wahitimu wa shahada ya Uzamivu kwenye mahafali hayo ya 48 ya Chuo Mkoani Morogoro. |
Akizungumza katika Mahafali ya 48 ya SUA Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, amesema Chuo kinaendelea kupata mafanikio katika utekelezaji wa jukumu lake la kuandaa wataalamu na kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
“Tunayo sababu ya kujipongeza kwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika
Chuo chetu mwaka hadi mwaka hususan katika kutekeleza jukumu letu la kuandaa
wataalamu na kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa,” alisema
Prof. Chibunda.
Prof. Chibunda amesema mahafali
hayo yamewakutanisha wahitimu 3,309 kutoka
programu 69, wakiwemo wanaume 1,774 na wanawake 1,535. Kati yao, wahitimu wa
Shahada za Kwanza ni 3,156, Shahada za Umahiri 62, Shahada za Uzamivu 22,
Stashahada za Uzamili wanne, Stashahada 60 na Astashahada watano.
Kwa mujibu wa Makamu Mkuu huyo
SUA imeanza kutekeleza hatua kadhaa muhimu chini ya Mpango Mkakati wa Chuo wa mwaka
2026–2031, ikiwemo kuanzishwa kwa programu
mpya tano zilizoidhinishwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU),
huku Chuo kikiendelea pia na utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi
ya Kiuchumi (HEET) kwa ajili ya kuimarisha miundombinu na mazingira ya
kujifunzia na kufundishia.
Katika eneo la utafiti, Prof.
Chibunda amesema SUA inaendelea kutekeleza miradi 116 ya utafiti katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa
na lengo la kuzalisha maarifa, teknolojia na ubunifu na kutoa suluhisho kwa
changamoto za kijamii na kiuchumi zinazolikabili Taifa na kwamba zaidi ya
watumishi 226 wako katika mafunzo ya umahiri na uzamivu ndani na nje ya nchi,
hatua inayolenga kuongeza ujuzi na weledi wa Chuo.
Akizungumzia hatua nyingine za
kimkakati, Prof. Chibunda amesema SUA imeanza shughuli za Kampuni ya Uzalishaji Mapato na Huduma za
Chuo inayolenga kuongeza vyanzo vya mapato na kuimarisha uwezo wa Chuo
kujitegemea kifedha.
Makamu huyo wa Mkuu wa Chuo
amesema Chuo kimepata idhini ya Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki
(IUCEA) kuendesha programu ya kikanda ya Shahada ya Umahiri ya Sayansi katika
Uhandisi na Usimamizi wa Umwagiliaji, hatua inayokiimarisha SUA kama kitovu cha
kikanda cha kuzalisha wataalamu wa umwagiliaji.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Baraza la SUA, Mhe. Andrew Massawe, amesema Baraza limeendelea kusimamia Chuo kwa kuzingatia
misingi ya weledi, uadilifu na uzalendo, huku likisisitiza matumizi sahihi ya
rasilimali na kuimarisha vyanzo vya mapato ya ndani kupitia miradi ya
kibiashara, huduma za ushauri na uwekezaji wa kimkakati.
“Baraza
la Chuo limeendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uadilifu na uzalendo,
likiwa na lengo kuu la kuhakikisha kwamba SUA inaendelea kuwa taasisi mahiri ya
elimu ya juu, utafiti na utoaji wa huduma bora kwa jamii,” alisema
Mhe. Massawe.
Aidha ameongeza kuwa katika
kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, Chuo kilitekeleza kwa wastani wa asilimia 80 ya shabaha
zilizopangwa, huku jumla ya Sh.
bilioni 125.775 zikitumika katika utekelezaji wa shughuli
mbalimbali.
“Baraza linaendelea kusimamia
Mradi wa HEET wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 62.776, unaohusisha ujenzi wa majengo manane katika
kampasi za Mizengo Pinda, Edward Moringe na Solomon Mahlangu, yakiwemo mabweni,
kumbi za mihadhara na maabara za mafunzo kwa vitendo” alisema Mhe. Massawe.
Mwenyekiti huyo wa Baraza la Chuo
pia amesema Baraza limeidhinisha kuanzishwa kwa Taasisi ya Mabadiliko ya Tabianchi na Bioanuai, inayolenga
kuimarisha tafiti na ubunifu katika kukabiliana na changamoto za mazingira
lakini pia Baraza hilo limeidhinisha Mpango Mkakati wa Sita wa SUA wa 2026–2031
pamoja na sera mbalimbali za TEHAMA, elimu mtandao, usimamizi wa kumbukumbu na
utoaji huduma na ushirikishwaji wa jamii.
Katika eneo la elimu, Massawe
amesema maboresho ya mitaala yamefanywa ili kuhakikisha programu za SUA
zinaendana na mahitaji ya soko la ajira, maendeleo ya sayansi na teknolojia
pamoja na mahitaji ya sekta za uzalishaji na kwamba asilimia 20 ya mafunzo itatolewa na wataalamu kutoka sekta za uzalishaji
na viwanda, huku TCU ikiwa tayari imeidhinisha mitaala mipya 111 ya kimkakati kuanza kutumika
katika mwaka wa masomo 2026/2027.
Katika nasaha zake kwa wahitimu
Mhe. Massawe amewataka kutumia elimu waliyoipata kubadilisha changamoto kuwa
fursa, na kuwa wabunifu katika kilimo, ufugaji, teknolojia na ujasiriamali
badala ya kutegemea ajira pekee.
“Tumieni
elimu mliyoipata kugeuza mawazo kuwa suluhisho, changamoto kuwa fursa na ndoto
kuwa mchango wenye maana kwa jamii huku mkihakikisha mnakuwa kizazi
kinachoongoza mageuzi kupitia sayansi, teknolojia na ubunifu na mzingatie
kuwa thamani ya elimu yenu itapimwa
zaidi kwa matokeo mtakayoacha katika maisha ya watu na maendeleo ya Taifa”
alisisitiza Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Mhe. Massawe.
Awali akizungumza kuhsu sherehe
za mahafali kabla ya kuanza rasmi mahafali hayo “MLAU” wa SUA Prof. Kalunde Sibuga amesema chimbuko la mahafali
lilianzia huko ulaya baada ya kuanzishwa kwa vyuo vikuu katika karne ya 12 hasa
baada ya vyuo vikuu vya kwanza kuanishwa na Makanisa.
“Viongozi hao wa makanisa ndio
walikuwa viongozi wakuu wa vyuo hivyo na katika kusherehekea upevukaji wa
wanafunzi hao yaani kuhitimu masomo walifanya sherehe na sherehe hiyo ndio
Mahafali ili kuwatunuku vyeti na ishara ya mamlaka ya kutunuku ni ile Rungu “SIWA”
ikiwa ni ishara ya wewe Mkuu wa Chuo Kutunuku vyeti na sio mtu mwingine”
alieleza Prof. Sibuga.
Aliongeza “Sherehe za Mahafali
zinakwenda sambamba na vazi maalumu na kwa kuzingatia kuwa vyuo vya kwanza
vilianzishwa na Makanisa na kama mjuavyo mavazi ya wakuu wa makanisa ni Kanzu
za aina mbalimbali hivyohivyo wahitimu wameendela kutumia vazi hilo ambalo sasa
tunaita Majoho kama kanzu za iana
fulani fulani zinazotofautiana kwa miraba na kofia na kamba ambazo zinatakiwa
kuwa kushoto kabla ya kutunukiwa”.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA MAHAFALI HAYO YA SUA.
| Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Mhe. Andrew W. Massawe akitoa salamu za Baraza kwenye mahafali hayo. |
| MLAU wa SUA Prof. Kalunde Sibuga akitoa maelezo ya awali ya maana ya mahafali na historia yake kwa wahitimu, Familia na wadau wa mahafali hayo. |
0 Comments