SUAMEDIA

ASP Komba aongoza mafunzo ya usalama SUA Kampasi ya Mizengo Pinda

Na: Mwandishi wetu

Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limeendelea kuimarisha ulinzi shirikishi kwa kutoa mafunzo ya ulinzi na usalama kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Kampasi ya Mizengo Pinda.

Mafunzo hayo yaliongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Kibaoni, ASP Komba, kwa lengo la kuwajengea wanafunzi uelewa kuhusu sheria za nchi, kujilinda na kutambua viashiria vya uhalifu wawapo chuoni na katika jamii.

Akizungumza na wanafunzi hao, ASP Komba amewahimiza kuzingatia masomo yao, kutumia mitandao ya kijamii kwa tahadhari na kujiepusha na uhalifu wa mtandaoni, utapeli pamoja na usambazaji wa taarifa za uongo.

Aidha, amewasisitiza kulinda mali zao, zikiwemo simu na kompyuta mpakato, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na makundi hatarishi, huku wakizingatia maadili na sheria za nchi.

ASP Komba ameeleza kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja, akiwahimiza wanafunzi kushirikiana katika kulinda wenzao na kutoa taarifa mapema kwa vyombo vya usalama wanapobaini viashiria vya uhalifu.

Kwa upande wao, wanafunzi wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa elimu hiyo iliyotolewa mwanzoni mwa masomo yao na kuahidi kuzingatia sheria, kulinda usalama wao na wa wengine, pamoja na kushiriki katika kujenga mazingira salama na tulivu ya kujifunzia.







Post a Comment

0 Comments