SUAMEDIA

Afrika Kusini kujenga mnara wa ukumbusho wa ukombozi Mazimbu

 Na:Ngolo Mboje

Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Noluthando Mayende-Malepe, amesema nchi yake inapanga kujenga mnara wa ukumbusho wa historia ya ukombozi wa Afrika Kusini katika eneo la Mazimbu, mkoani Morogoro, kwa lengo la kuenzi mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa nchi hiyo.



Balozi Mayende-Malepe amesema hayo wakati wa ziara yake katika eneo la urithi wa kihistoria la Mazimbu, lililopo Kampasi ya Solomon Mahlangu ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambapo alikutana na viongozi kujadili mpango wa utekelezaji wa mradi huo.

Amesema Tanzania ilitoa hifadhi na msaada kwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini waliokimbia mfumo wa ubaguzi wa rangi wa Apartheid, hivyo ujenzi wa mnara huo utasaidia kuhifadhi historia hiyo muhimu na kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, amesema mradi huo unapaswa kuwa zaidi ya mnara wa ukumbusho kwa kujumuisha shughuli za utamaduni, sanaa, michezo na biashara zitakazochochea utalii na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi.

Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Maulid Mwatawala, aliyemwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Raphael Chibunda, ameahidi ushirikiano wa chuo hicho katika kufanikisha mradi huo na kuhakikisha urithi wa kihistoria wa Mazimbu unalindwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Prof. Mwatawala amesema eneo la Mazimbu lina nafasi muhimu katika historia ya ukombozi wa Afrika Kusini, ikiwemo historia ya harakati za Chama cha ANC na mkutano wake uliofanyika Morogoro mwaka 1969.

Amesisitiza umuhimu wa kuhifadhi maeneo hayo ili kuendeleza uelewa wa mchango wa Tanzania katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Aidha, amependekeza timu ya taifa ya soka ya Afrika Kusini itakayotembelea Tanzania kwa ajili ya mashindano ya AFCON ipangiwe kutembelea eneo la Mazimbu ili kujifunza historia ya ukombozi na kutambua mchango wa Tanzania katika harakati hizo.

Mradi huo unatarajiwa kuwa kichocheo cha kukuza utalii wa kihistoria mkoani Morogoro, kuhifadhi urithi wa ukombozi wa Afrika Kusini na kuimarisha zaidi urafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini.








Post a Comment

0 Comments