Na: Farida Mkongwe
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam
Kigoma Malima, amewataka wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga na
Morogoro kujitokeza kwa wingi kushiriki Maonesho ya Wakulima na Wafugaji ya
Nanenane Kanda ya Mashariki yatakayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, mjini Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja hivyo, Malima amesema maonesho ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa kutokana na kuwakutanisha wadau mbalimbali, kuonesha ubunifu na teknolojia za kisasa, pamoja na kufungua fursa za masoko katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.
“Maonesho haya yana fursa
nyingi kwa wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla,
tunawahimiza wananchi wa Kanda ya Mashariki na maeneo mengine kujitokeza kwa
wingi ili kujifunza na kutumia fursa zitakazopatikana,” amesema Malima.
Amesema zaidi ya watu 250,000 kutoka ndani na nje ya Kanda ya Mashariki wanatarajiwa kutembelea maonesho hayo, ikilinganishwa na watu 150,000 waliohudhuria mwaka jana.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa
amesema maandalizi ya maonesho hayo yamekamilika kwa asilimia 98, huku tiketi
za kuingia viwanjani zikitarajiwa kutolewa kwa njia ya kidigitali kwa mara ya
kwanza ili kupunguza foleni na usumbufu kwa wageni.
Waziri wa Viwanda na Biashara,
Mhe. Judith Salvio Kapinga, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa
maonesho hayo yatakayoanza Agosti 1, 2026, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo,
“Tambua Soko; Ongeza Tija, Kutekeleza Dira 2050.”


.jpeg)

0 Comments