Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Imeelezwa kuwa Ubia kati ya
Serikali na Sekta Binafsi (PPP),Weledi wa watu kwenye usimamizi wa miradi na Taasisi
pamoja na maarifa kwenye sekta za uzalishaji na utoaji huduma ndio nguzo inayoweza
kuifanya Tanzania kufikia malengo ya Mpango
wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) wa kipindi cha
2026/27–2030/31.
| Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPPC) Bwana David Kafulila wakati akitoa mhadhara katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo. |
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha Ubia kati ya Serikali na
Sekta binafsi (PPPC) Bwana David Kafulila wakati akitoa mhadhara wa wazi kwenye
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kuhusu nafasi ya ushirikiano kati ya
Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika kuleta mageuzi ya kilimo kwa muktadha wa
malengo ya Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) wa
kipindi cha 2026/27–2030/31.
Amesema malengo ya PPP ni kuvuta
mitaji ya sekta binafsi kwa kuipa nafasi ya kuwekeza kwenye miradi na utoaji wa
huduma,kuongeza matumizi makubwa ya teknolojia na ubunifu kwakuwa sekta binafsi
zina nafasi kubwa katika kutumia teknolojia kwa haraka pamoja na kuwa na weledi
katika kusimamia makampuni na miradi inayokabidhiwa ili kuongeza ufanisi na
tija kwao.
“Duniani huko hasa nchi
zilizoendelea zinashindana kwa ubora wa watu wake katika kufanya kazi na
matumizi ya teknolojia za juu katika kutoa huduma, kuongeza ufanisi na kuleta
faida, jambo hili linakwenda sambamba na kuhakikisha watu wake wanakuwa na
maarifa na lishe lakini nchi hizo zikihimiza swala la ubia kati ya sekta ya
Umma na sekta binafsi ili kuchochea maendeleo” alieleza Kafulila.
Mkurugenzi huyo wa PPPC amesema
swala la PPP sio jambo la Tanzania bali ndio agenda ya dunia na nchi
zilizoendelea na katika miaka mitano tangu kuanzishwa kwa Ubio huo hapa nchini,
Tanzania imeweza kukuza thamni yake kutoka Trilioni 2 hadi kufikia zaidi ya 8
jambo ambalo limechangiwa na serikali kufungua milango kwa sekta binafsi
kushirikiana na sekta ya umma.
Aidha bwana Kafulila amesema PPP
inatoa fursa kwa sekta binafasi kufanya shughuli mbalimbali za kibiashara na
kiuchumi ambazo zinatakiwa kufanywa na serikali ili yenyewe ibaki na zile za
kihuduma zaidi ambazo sekta binafsi haiwezi kutokana na kutokuwa na faida sana
na kwa kufanya hivyo serikali inajipunguzia mzigo huku nchi ikipata maendeleo.
Amesema Chuo Kikuu cha Sokoine
kina mchango mkubwa katika kusaidia eneo la maarifa hasa ikizingatiwa kuwa
sekta hiyo inachangia ajira kwa wananchi kwa zaidi ya asilimia 65 huku asilimia
70 ya watanzania wanaishi vijijini hivyo bila kuwa na wataalamu wa kutosha ni
vigumu kuongeza tija kwenye sekta hiyo na kapambana na umasikini.
Awali akizungumza kwa niaba ya
Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Raphael Chibunda kabla ya kumkaribisha kuongea na
wanajumuiya ya SUA, Naibu Mkamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
Mipango fedha na Utawala Prof. Amandus Muhairwa amesema Chuo hicho kinashiriki
kwa asilimia kubwa katika kutekeleza mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa kuchangia
katika kuzalisha wataalamu, Kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu katika
sekta mbalimbali zinazohusiana na kilimo na sayansi za kilimo.
| Naibu Mkamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Mipango fedha na Utawala Prof. Amandus Muhairwa akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kutoa mhadhara. |
“Uamuzi wa PPPC kufanya mhadhara
huu chuoni hapa haukuja kwa bahati mbaya bali ni kutokana na kituo hicho
kutambua nafasi ya SUA katika kutekeleza Mpango huo wa maendeleo na katika
nafasi yake ya kuzalisha wataalamu hodari na mahiri wanye mchango mkubwa katika
kukuza sekta ya Umma na sekta binafsi kwa kuzalisha ajira na kuleta maendeleo
ya watu” Alibainisha Muhairwa.
Aliongeza “Nchi zilizoendelea
sana kama China zimetumia sana Elimu, Tafiti. Ubunifu, Kilimo na Teknolojia
katika kujenga uchumi imara hali ambayo inasaidia kuongeza tija katika
uzalishaji wa bidhaa na teknolojia mbalimbali kwani serikali inatoa miongozo na
sera huku sekta binafsi ikitoa mitaji na teknolojia”.
Prof. Muhairwa amesema Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo SUA kipo tayari na kinaendelea kusaidia utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka
Mitano (FYDP IV) wa kipindi cha 2026/27–2030/31 kupitia kuleta mageuzi ya sekta ya Kilimo.
Akitoa
shukrani Rasi wa Ndaki ya Kilimo Dkt. Nyambilila Amuri amesema Mhadhara huo
umeleta faida kubwa kwa wanajumuiya wa SUA kwa kukutanisha Watafiti,Walimu,
Wanafunzi na wadau wengine hasa katika kuelewa dhana nzima za PPP kwa kina na
kutoa nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali ambayo yamesaidia wanazuoni hao
kuona nafasi yao katika kutekeleza mpango huo wa maendeleo ya Taifa kupitia
PPP.
“Sote
tutakubaliana kuwa wasilisho la Mkurugenzi wa PPPC limegusa kila kozi
zinazofundshwa hapa chuoni hivyo kila mmoja anaweza kusoma akijitazama nafasi
yake kwenye kushiriki kwenye mpango huu wa nne wa taifa kupitia maarifa
anayoyapata chuoni hapa, hivyo tujipange mapema kuwaza namna ya kushiriki
uwekezaji wa ubia na serikali kwenye nyanja mbalimbali” Alisema Dkt. Amuri.
MATUKIO KATIKA PICHA WASHIRIKI WA MHADHARA HUO WAKIFUATILIA NA KUULIZA MASWALI.
0 Comments