Na: Mwandishi wetu.
Mtanzania Bi. Rehema Katuga
kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria nchini (OCPD) ameibuka mshindi katika
uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Uongozi na Usimamizi la Chama cha wataalamu wa
Uandishi wa sheria wa Jumuiya ya Madola (CALC), na kuwa mmoja wa wawakilishi wa
Afrika katika baraza hilo.
![]() |
| Bi. Rehema Katuga ambaye ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Urekebu Utafiti na Mafunzo kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) |
Baraza hilo lenye wawakilishi
wawili kutoka kila bara linasimamia na kufanya maamuzi muhimu kuhusu uendeshaji
wa chama hicho cha kitaaluma cha wataalamu wa uandishi wa sheria katika nchi
wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Bi. Katuga ameibuka mshindi
katika uchaguzi uliowahusisha wagombea wanne kutoka Afrika, wakiwemo wagombea
wawili kutoka Afrika Kusini, mmoja kutoka Namibia na yeye akiwa muwakilishi
pekee kutoka Tanzania, hivyo kuiwezesha Tanzania kupata nafasi ya uwakilishi
katika chombo hicho muhimu cha kitaaluma.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa
CALC, imeelezwa kuwa chama hicho ni miongoni mwa vyama vya kitaaluma
vinavyosimamiwa na Jumuiya ya Madola na kina jukumu la kuimarisha ushirikiano
miongoni mwa wataalamu wa uandishi wa sheria katika nchi wanachama.
“CALC inalenga kuimarisha uwezo
wa wataalamu hao katika kuandaa sheria bora zinazoweza kutafsiri sera za
Serikali na kubeba mageuzi mbalimbali yanayohitajika katika nchi, huku
ikisisitiza ushirikiano katika mafunzo, kubadilishana uzoefu, programu za
mafunzo kwa vitendo (attachments), matumizi ya teknolojia katika uandishi wa
sheria na kuendeleza mbinu bora za uandishi wa sheria” alieleza Bi Katuga.
Aliongeza “Lakini pia cham hiki
kina Baraza la uongozi linalojumuisha viongozi wakuu pamoja na wawakilishi
kutoka mabara mbalimbali ambao ndio sisi tuliochaguliwa sasa, ambao kwa pamoja
hushiriki katika kutoa mwelekeo na kufanya maamuzi kuhusu maendeleo ya taaluma
ya uandishi wa sheria”.
Muwakilishi huyo wa Tanzania na
Afrika amesema kupitia nafasi hiyo aliyoipata itamuwezesha kuchangia kutoa
fursa kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kuimarisha ushirikiano wa wataalamu wa
uandishi wa sheria, kubadilishana maarifa na uzoefu na nchi nyingine za Jumuiya
ya Madola, pamoja na kujifunza na kutumia mbinu bora za kisasa katika uandishi
wa sheria.
Aidha amesema anatarajiwa
kushiriki kikamilifu katika kuunganisha wataalamu wa uandishi wa sheria barani
Afrika, kukuza taaluma hiyo na kuchangia katika juhudi za kuboresha ubora wa
sheria kupitia uandishi wenye weledi, uwazi na ufanisi.
Kwa Tanzania uwakilishi huo pia
unaongeza nafasi ya nchi kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu
maendeleo ya taaluma ya uandishi wa sheria na kunufaika na fursa za mafunzo, kujengea
uwezo wataalamu wa fani hiyo nchini na ubadilishanaji wa teknolojia na uzoefu,
hatua inayoweza kusaidia kuimarisha ubora wa mchakato wa uandaaji wa sheria
nchini.
Matokeo hayo ya Uchaguzi
yalitangazwa kwenye mkutano Mkuu wa Chama hicho uliofanyika tarehe 19 mwezi huu
nchini Singapore.

0 Comments