SUAMEDIA

SUA kuonesha mbinu zitakazoongeza tija na kipato Nanenane 2026

 Na: Ngolo Mboje

Wakulima, wafugaji na wavuvi nchini wamehimizwa kutembelea mabanda ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanayoanza Agosti 1, 2026, ili kujifunza teknolojia na mbinu bora za kisasa za uzalishaji, kupata ushauri wa kitaalamu na huduma mbalimbali zitakazowasaidia kuongeza tija na kipato.

Akizungumza na SUA Media, Mkuu wa Kitengo cha Ugani cha SUA, Dkt. Emmanuel Timothy Malisa, amesema Chuo kimekamilisha maandalizi ya kushiriki maonesho hayo kwa kuandaa huduma mbalimbali za elimu na ushauri zitakazowanufaisha wakulima, wafugaji, wavuvi na wananchi kwa ujumla.

Dkt. Malisa amesema wananchi watakaotembelea mabanda ya SUA watapata elimu kuhusu uzalishaji wa mazao mbalimbali, yakiwemo mpunga na mchicha, pamoja na mbinu bora za ufugaji na utunzaji wa aina mbalimbali za mifugo.

“Tumejipanga kikamilifu kuhakikisha kila atakayefika katika mabanda ya SUA anapata elimu ya kina kuhusu teknolojia na mbinu bora za uzalishaji. Pia tunawaomba wananchi wanaohitaji kupima udongo waje na sampuli zisizopungua tano za udongo kwa ajili ya kupimwa bila malipo ili wapate ushauri sahihi kuhusu afya ya udongo wao,” amesema Dkt. Malisa.

Mbali na elimu ya kilimo na ufugaji, SUA itatoa ushauri kuhusu lishe bora kwa watoto, kinga na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukiza pamoja na afya ya udongo.

Aidha, wanafunzi wa masomo ya Amali kutoka Shule ya Sekondari Mafiga, mkoani Morogoro, watapatiwa mafunzo ya vitendo kuhusu ufugaji na utunzaji wa mifugo ili kuwajengea ujuzi utakaowawezesha kujiajiri au kushindana katika soko la ajira baada ya kuhitimu masomo yao.

Maonesho ya Nanenane hufanyika kila mwaka kuanzia Agosti 1 hadi 8 na hukutanisha wadau wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuonesha teknolojia mpya, kubadilishana uzoefu na kutoa elimu inayochochea ongezeko la uzalishaji, usalama wa chakula na maendeleo ya uchumi wa wananchi.

Maonesho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, “Tambua Soko; Ongeza Tija Kutekeleza Dira 2050.”





Post a Comment

0 Comments