Na: Ayoub Mwigune
Ufugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kata ya Igima, Wilaya ya
Wanging’ombe mkoani Njombe, umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mabadiliko ya
kiuchumi kwa wananchi, kufuatia kuongezeka kwa uzalishaji na kuboreka kwa ubora
wa maziwa kutokana na elimu na tafiti zinazotolewa na wataalamu kutoka Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).
Akizungumza kuhusu maendeleo ya ufugaji katika kata hiyo, Afisa Mifugo wa Kata ya Igima, Shazi Moses Okala, amesema kata hiyo ina zaidi ya wafugaji 300 wa ng’ombe wa maziwa, wakiwa na zaidi ya ng’ombe 700. Amesema kwa sasa wafugaji hao huzalisha zaidi ya lita 2,500 za maziwa kwa siku.
Amesema maziwa yanayozalishwa hukusanywa kupitia vituo vya
ukusanyaji kabla ya kupelekwa kwenye kituo cha kupoozea, na baadaye
kusafirishwa kwa ajili ya usindikaji.
Okala amesema kabla ya kuanza kwa elimu na utafiti
unaotolewa na wataalamu wa SUA kupitia Mradi wa NANOCOM, wafugaji walikuwa
wakikabiliwa na changamoto mbalimbali, hususan ugonjwa wa homa ya kiwele kwa
ng’ombe wa maziwa, unaosababisha kupungua kwa ubora wa maziwa.
Ameeleza kuwa hali hiyo ilikuwa ikisababisha maziwa mengi
kuchachuka na kupoteza ubora wake, jambo lililokuwa likiwaathiri wafugaji
kiuchumi. Hata hivyo, amesema changamoto hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa baada
ya wafugaji kupewa elimu kuhusu usafi wa mabanda, ukamuaji sahihi na mbinu bora
za ufugaji.
“Kwa sasa wafugaji wengi wamepata uelewa mkubwa kuhusu namna bora ya kutunza ng’ombe wa maziwa, kuzingatia usafi wa mabanda na kudhibiti magonjwa. Hali hii imesaidia kuboresha afya ya mifugo na kuongeza ubora wa maziwa,” amesema Okala.
Ameongeza kuwa elimu hiyo imechangia kuongeza uzalishaji wa
maziwa na kipato cha wafugaji, ambapo kwa sasa maziwa mengi yanakidhi viwango
vya soko tofauti na ilivyokuwa awali.
Kwa upande wake, mfugaji na kiongozi wa kikundi cha Beach
Group, Bi. Liones Richard,
amesema ufugaji wa ng’ombe wa maziwa umebadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa
tangu alipoanza shughuli hiyo mwaka 2007 akiwa na ng’ombe mmoja pekee.
Bi. Liones amesema kwa sasa anamiliki ng’ombe wanne, ambapo
kila ng’ombe ana uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita 20 za maziwa kwa siku.
Amesema mafanikio hayo yametokana na matumizi ya mbinu bora za ufugaji pamoja
na ushauri wa kitaalamu anaoupata kutoka kwa wataalamu wa mifugo.
Amesema kupitia elimu hiyo, ameweza kuboresha lishe ya mifugo, afya ya ng’ombe na usafi wa mabanda, hatua iliyosaidia kuongeza uzalishaji wa maziwa na kipato cha familia yake.
“Ufugaji wa ng’ombe wa maziwa umenisaidia sana. Kupitia
shughuli hii nimeweza kujenga nyumba bora na kusomesha watoto wangu.
Nawahamasisha wanawake, vijana na wafugaji wengine kuuchukulia ufugaji huu kama
fursa muhimu ya kujikwamua kiuchumi,” amesema Bi. Liones.
Ameongeza kuwa ufugaji wa ng’ombe wa maziwa unaweza
kubadilisha maisha ya wananchi endapo utafanyika kwa weledi, nidhamu na kwa
kuzingatia maarifa sahihi ya kitaalamu.
Kwa ujumla, elimu na utafiti unaotolewa na SUA kupitia Mradi
wa NANOCOM umeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kuboresha ufugaji wa
ng’ombe wa maziwa, kuongeza ubora wa maziwa na kuinua kipato cha wafugaji
katika Kata ya Igima na maeneo mengine ya mkoa wa Njombe.




0 Comments