Na: Vumila Kondo
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeandika rekodi ya kipekee nchini baada ya kutangaza kufanikiwa kupata Hati Safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka 20 mfululizo.
Rekodi hiyo ya kihistoria ya
uwajibikaji na usimamizi bora wa fedha imetangazwa wakati wa Mahafali ya 47 ya
chuo hicho yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya Edward Moringe.
Mbali na rekodi hiyo ya CAG, SUA
imeendeleza ubabe wake wa kifedha baada ya kutunukiwa tuzo ya kuwa taasisi ya
juu ya elimu inayoongoza kwa uandaaji bora wa hesabu nchini na Bodi ya NBAA kwa
miaka mitatu mfululizo.
Mafanikio haya makubwa yameongeza
chachu ya furaha katika mahafali hayo yaliyoshuhudia jumla ya wahitimu 877 wakitunukiwa
shahada za Uzamivu, Uzamili, Shahada za Kwanza, Stashahada za juu, Stashahada
na Astashahada mbalimbali chini ya uongozi wa Mkuu wa Chuo, Jaji Joseph Sinde
Warioba.
Akiwasilisha ripoti hiyo ya
mafanikio ya fedha na utawala bora mbele ya hadhara, Makamu Mkuu wa Chuo,
Profesa Raphael Chibunda amesema:
"Tumendelea kuimarisha
nidhamu katika majukumu ya chuo, na hatua hiyo imekiwezesha chuo chetu kupata
hati safi kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Hii
inaendeleza rekodi yetu ya hati safi kwa dhihirisho la miaka 20 mfululizo."
Uchambuzi wa kitaaluma unaonyesha
kuwa wahitimu wa Shahada za Kwanza (Bachelor) walikuwa 698, Shahada za Umahiri
(Masters) 132, Shahada za Uzamivu 19, Stashahada 141, na Astashahada 23.
Katika hatua nyingine ya
maendeleo, Profesa Chibunda ametangaza kuwa chuo kipo hatua za mwisho kuzindua
kituo chake rasmi cha runinga cha SUA TV, ambacho kitakuwa nyanja ya
kimkakati ya kusambaza teknolojia za kisasa za kilimo, mifugo, na uvuvi kwa
jamii.
Pia, amejivunia vijana wa SUA
Innovation Hub kupitia timu za Snackers Square na Eco Mushroom
kwa kushika nafasi ya kwanza kitaifa kwenye mashindano ya Youth Ignite
Student Founders Fellowship, akisisitiza kuwa chuo kimebobea katika
kuwajenga wanafunzi kiuandishi na kiubunifu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Baraza la Chuo, Ndugu Andrew Masawe, akizungumza kuhusu dira na majukumu ya
Baraza katika kusimamia chuo, ameeleza kuwa Baraza limeendelea kuboresha sura
na utendaji wa Chuo kwa ujumla.
"Baraza limeendelea kwa
kiasi kikubwa kutekeleza mambo mengi makubwa yanayolenga kuboresha sura na
utendaji wa chuo kwa ujumla Pia, Baraza limeidhinisha nyaraka muhimu za
kimkakati ikiwemo miongozo ya ukuzaji wa machapisho ya Maktaba ya Taifa ya
Kilimo ya mwaka 2025."Amesema Massawe.




0 Comments