Na: Vumilia Kondo
Katika ulimwengu wa sasa ambapo
teknolojia inakua kwa kasi, redio bado imebaki kuwa nyenzo imara na ya gharama
nafuu katika kufikisha maarifa ya kilimo kwa wakulima vijijini kutokana na
uwezo wake wa kuvuka vikwazo vya elimu na gharama.
Utafiti huo umehusisha wakulima
204 kutoka kata za Mlali, Wami-Dakawa, na Mzumbe, umebaini kuwa redio hiyo ni
chanzo kikuu cha habari ambacho kimebadilisha mfumo wa kilimo kwa kiasi kikubwa
kupitia maudhui yanayozingatia utafiti wa kisayansi na ushauri wa kitaalamu.
Matokeo ya utafiti huo yameonesha
takriban asilimia 91.6 ya wakulima walikiri kuwa mbinu zao za ulimaji
zimeboreka kupitia vipindi vya SUA FM.
"Uchambuzi umeonesha kuwa asilimia 91.6 ya wakulima walikiri kuwepo kwa maboresho katika mbinu zao za kilimo kutokana na vipindi vya SUA FM, hususan katika mbinu za ukuzaji wa mazao, matumizi ya mbegu bora, utabiri wa hali ya hewa, na udhibiti wa wadudu, amesema Gwabara.
Aidha, zaidi ya asilimia 80 ya wakulima wameonesha
kuridhishwa na maudhui yanayotolewa, huku wengi wao wakieleza kuwa habari hizo
huwafikia kwa wakati mwafaka kulingana na kalenda ya msimu wa kilimo.
Pamoja na mafanikio hayo,
utafiti umeibua tofauti za kundi la wasikilizaji ambapo wakulima vijana
wameonekana kuitegemea zaidi redio hiyo kama chanzo chao kikuu cha maarifa.
Hata hivyo, Gwabara amebainisha
kuwa kuna changamoto zinazokwamisha ufanisi kamili wa redio hiyo katika kuleta
mageuzi ya kilimo, hasa kutokana na kukosekana kwa baadhi ya taarifa muhimu za
kiuchumi.
"Licha ya SUA FM kuwa chanzo kikuu, utafiti ulibaini kuwepo kwa mapengo ya habari katika maeneo ya mikopo ya kilimo, upatikanaji wa masoko, na usimamizi wa mazao baada ya kuvuna, mambo ambayo yamepunguza ufanisi wa jumla kwa mkulima mmoja mmoja," amesema Gwabara.
Changamoto nyingine zilizotajwa
ni pamoja na usikivu mdogo wa mawimbi ya redio katika maeneo ya pembezoni na
muda mfupi wa matangazo ambao wakati mwingine hauendani na nafasi ya mkulima
akiwa nyumbani.
Ili kuifanya SUA FM kuwa injini
kamili ya mabadiliko, utafiti huo umependekeza kuwa watayarishaji wa vipindi
wanapaswa kutanua wigo wa maudhui yao kwa kujumuisha habari za kina kuhusu
mikopo, masoko, na teknolojia mpya za kisasa ili kuwavutia wasikilizaji wa rika
zote.
"SUA inapaswa kuimarisha usikivu wa mawimbi ya redio kwa kuboresha miundombinu ya urushaji matangazo katika maeneo ya mbali ya Mvomero ambapo utafiti umebaini kuwa usikivu ni changamoto kubwa."
Pia, ameshauri kutolewa kwa ratiba za vipindi mara kwa mara na kuvirudia
nyakati za jioni ili kuhakikisha kila mkulima anapata fursa ya kujifunza na
kuboresha tija katika uzalishaji wa mazao kama mahindi, mpunga, na mbogamboga.




0 Comments