SUAMEDIA

SUA yatoa mafunzo ya ufugaji bora wa nguruwe kuongeza tija kwa wafugaji

Na: Vumilia Kondo

Ufugaji wa nguruwe ni miongoni mwa miradi inayokua kwa kasi nchini  kutokana na uwezo wake wa kuinua kipato cha kaya kwa muda mfupi.

Hata hivyo, changamoto za magonjwa, lishe duni, ukosefu wa elimu ya kitaalamu na masoko zimekuwa zikirudisha nyuma juhudi za wafugaji wengi.

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza (ICE) ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), imeendesha mafunzo maalum ya ufugaji bora wa nguruwe yaliyowaleta pamoja wataalamu, wafugaji wenye uzoefu pamoja na watu wanaotarajia kuanza mradi huo kutoka mikoa nane nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Prof. Raphael Chibunda, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Kujiendeleza SUA, Dkt. Devotha Mosha, amesema ufugaji wa nguruwe una nafasi kubwa katika kuinua kipato cha kaya na kuchangia usalama wa chakula, hivyo ni muhimu wafugaji kupata elimu ya msingi kabla ya kuanza shughuli hiyo.

“Tunashauri wafugaji wa nguruwe, kuku na sungura kupata mafunzo ya msingi kabla ya kuanza,hii inawasaidia kufikia malengo ya kukuza kipato na kuimarisha usalama wa chakula,” amesema Dkt. Mosha.

Kwa upande wake, mtaalamu wa mifugo kutoka SUA, Prof. Faustine Lekule, amesema sekta ya ufugaji wa nguruwe inakabiliwa na changamoto kuu nne ambazo ni magonjwa, hasa yasiyo na tiba kama homa ya nguruwe ya Afrika, gharama na ubora wa chakula, ukosefu wa elimu kwa wafugaji pamoja na changamoto za masoko.

Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwapa washiriki uelewa wa kina kuhusu mbinu bora za ufugaji kuanzia lishe, uzalishaji, udhibiti wa magonjwa hadi usimamizi wa shamba, ili waweze kufuga kwa tija na kupata faida.

“Mafunzo haya yanalenga kuwapa washiriki uelewa wa kina wa mbinu bora za ufugaji kuanzia lishe, uzalishaji hadi usimamizi wa shamba, mambo ambayo yatawasaidia kuona faida za ufugaji wa nguruwe,” amesema Prof. Lekule.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu waliyoipata imewapa mwanga mpya kuhusu namna bora ya kuendesha ufugaji wa nguruwe kwa kuzingatia kanuni za kitaalamu.

Mmoja wa washiriki hao, Anastasia Seleli, amesema ingawa bado hajaanza kufuga, ameamua kushiriki mafunzo hayo ili ajipange vizuri kabla ya kuingia kwenye biashara hiyo.

“Nilikuwa na mambo machache kichwani, lakini hapa napata mengi zaidi ya niliyoyatarajia. Mafunzo haya ni mkombozi kwangu kwa sababu yananisaidia kujua namna ya kuanza kwa usahihi,” amesema Anastasia.

Naye Blasius Kigeso kutoka Dodoma amesema aliamua kushiriki mafunzo hayo kutokana na changamoto za magonjwa pamoja na ukosefu wa ujuzi sahihi miongoni mwa wafugaji wengi.

“Wafugaji wengi hutegemea uzoefu wa kawaida bila msingi wa kitaalamu. Elimu ninayopata itanisaidia kupunguza hasara na kuongeza tija katika shughuli zangu,” amesema Blasius.

Kwa ujumla, mafunzo hayo yanatoa nafasi kwa washiriki kujifunza mbinu za kisasa za ufugaji, ikiwemo uchaguzi wa mbegu bora za nguruwe, uzalishaji kwa njia ya kisasa kama uhimilishaji, pamoja na matumizi ya teknolojia kama kamera katika kusimamia mifugo.

Mbinu hizo zinatajwa kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ubora wa nyama, kasi ya ukuaji wa mifugo na tija kwa ujumla.

Kupitia mafunzo hayo, SUA imeendelea kusisitiza umuhimu wa wafugaji kupata elimu ya kitaalamu ili kuhakikisha ufugaji unakuwa endelevu, wenye tija na wenye manufaa kwa kaya na taifa kwa ujumla.






Post a Comment

0 Comments