SUAMEDIA

RC Morogoro ahamasisha wafanyakazi kujituma ili kufikia Dira ya Taifa 2050

 Na : Ayoub Mwigune - Gairo

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro amewahimiza wafanyakazi kufanya kazi kwa staha, kujituma na kuzingatia maadili ya kazi ili kuchangia kikamilifu katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.



Ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi, 2026) yaliyofanyika kimkoa katika Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro.

Akizungumza katika hafla hiyo, amesema Tanzania ni nchi yenye malengo makubwa ya maendeleo, na mafanikio yanayoendelea kupatikana ni matokeo ya uongozi thabiti wa Serikali pamoja na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na vyama vya wafanyakazi.

 Aidha, amewahimiza wananchi kufuatilia taarifa za habari ili kufahamu changamoto zinazoikabili nchi yao na namna ya kushiriki katika kuzitatua.

Amesisitiza kuwa Serikali ipo karibu na wafanyakazi na iko tayari kupokea na kushughulikia changamoto zao na kuwa baadhi ya madai ya wafanyakazi tayari yamepatiwa ufumbuzi, huku mengine yakiendelea kufanyiwa kazi, kwani changamoto hizo haziwezi kumalizika kwa wakati mmoja bali zinahitaji juhudi endelevu.

Kuhusu maslahi ya wafanyakazi, amesema nyongeza ya mishahara huzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo pato la taifa. Aidha, amewataka waajiri kuhakikisha wanalipa madeni ya wafanyakazi, hususan wastaafu, na kusisitiza matumizi ya njia za upatanishi katika kutatua migogoro ya kikazi ili kudumisha amani na utulivu mahali pa kazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa wa Morogoro, Bw. Elius Yuda Mtungirwa, amesema wafanyakazi wataendelea kuwa wabunifu, kujituma na kuzingatia kanuni na miongozo ya kazi huku wakidumisha amani na mshikamano.

Kwa upande wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wafanyakazi hodari wa mwaka 2026, Bw. Kajura Magoma na Dkt. Nkuba Mbeho, wamesema mafanikio yao yametokana na kujituma kazini, kutimiza majukumu kwa ufanisi na kujenga nidhamu ya kazi, pamoja na uwezo wa kukabiliana na changamoto katika maeneo yao ya kazi.



 

 

Post a Comment

0 Comments