SUAMEDIA

SUA yasisitiza ushirikiano na kujituma kazini, yawatunuku wafanyakazi bora Mei Mosi

 Na: Ngolo Mboje- Morogoro.

Watumishi wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamehimizwa kufanya kazi kwa bidii, kuimarisha utendaji wao na kuchangia kwa dhati maendeleo ya chuo pamoja na jamii kwa ujumla.



Wito huo umetolewa na Prof. Amandus Muhairwa, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala, kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi, 2026) yaliyofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe, mkoani Morogoro.

Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Muhairwa amebainisha kuwa SUA ni Taasisi ya mfano katika tafiti bunifu na utoaji wa huduma kwa jamii na kwamba Chuo hicho kina mazingira rafiki ya kazi, mifumo inayozingatia haki, uwazi na uwajibikaji, ambayo ni msingi muhimu wa kujenga taasisi yenye ushindani na mchango halisi katika maendeleo ya jamii.

Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuipatia SUA ajira mpya 263, hatua ambayo imeongeza nguvu kazi chuoni hapo, ameongeza kuwa chuo kinaendelea kuboresha upatikanaji wa vifaa vya kazi na kuimarisha mifumo ya ununuzi ili kuongeza ufanisi na kuendeleza dhamira ya pamoja ya kujenga SUA iliyo bora zaidi.

Katika hatua nyingine, Prof. Muhairwa amewapongeza wafanyakazi wote, hususan waliotunukiwa tuzo mbalimbali, kwa juhudi na kujituma kwao katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku na kusema mchango wao umeiwezesha SUA kuendelea kuwa kitovu muhimu cha elimu ya kilimo nchini.

Kwa upande wao, Mwenyekiti wa RAAWU tawi la SUA, Bw. Faraja Kamendu, pamoja na Mwenyekiti wa THTU tawi hilo, Bw. Nikson Mkiramwene, wameipongeza Menejimenti ya Chuo na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutambua mchango wa wafanyakazi na kushughulikia baadhi ya changamoto, ikiwemo ulipaji wa deni la wanataaluma na huduma za matibabu kwa wafanyakazi wa SUA.

Naye, Prof. Herzon Nonga, akitoa shukrani kwa niaba ya wafanyakazi bora, ameushukuru uongozi wa SUA kwa kutambua juhudi zao kupitia utoaji wa tuzo, na kuwataka wafanyakazi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya mustakabali na maendeleo ya chuo.

Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani hufanyika kila mwaka tarehe 1 Mei, yakilenga kutambua mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

0 Comments