SUAMEDIA

Serikali kuwasilisha Rasimu ya Taarifa ya Hali ya Haki za Binadamu

 Na Vumilia Kondo

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeingia katika hatua ya lala salama ya kuhakiki Rasimu ya Taarifa ya Hali ya Haki za Binadamu nchini (UPR), itakayowasilishwa mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Zainab Katimba akizungumza katika mkutano

Akifungua kikao kazi cha uhakiki wa rasimu hiyo mkoani Morogoro, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Zainab Katimba amebainisha kuwa mchakato huo ni kielelezo cha utashi wa kisiasa wa Tanzania katika kuheshimu utu na misingi ya kisheria.

Naibu Waziri ameeleza kuwa katika mzunguko wa tatu uliopita, Tanzania ilikubali kutekeleza jumla ya mapendekezo 187, jambo ambalo ameliita kuwa ni ahadi ya kitaifa na kielelezo cha utayari wa nchi katika kujitathmini.

"Taarifa mnayoandaa si taarifa ya kawaida, ni taswira halisi ya namna Serikali inavyotekeleza wajibu wake, uimara wa taasisi zetu na athari za kazi zetu katika maisha ya wananchi."Amesema Mheshimiwa Katimba

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Richard Kilanga ametoa ufafanuzi wa kiufundi kuhusu mfumo huo akibainisha kuwa huo ni mchakato wa kipekee ambapo nchi inafanyiwa tathmini na nchi wanachama wenzake wa Umoja wa Mataifa.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Haki za Binadamu kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Richard Kilanga akizungumza na washiriki

"Tanzania imekuwa ikishiriki kikamilifu katika mchakato wa UPR tangu kuanzishwa kwake na sasa tupo katika mzunguko wa nne. Katika mzunguko uliopita, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikubali kutekeleza jumla ya mapendekezo 187." Amesema Richard Kilanga Mkurugenzi msaidizi wa Katiba na sheria.

Ripoti inayohakikiwa sasa imejikita katika maeneo ya kipaumbele ikiwemo uhuru wa kujieleza, ulinzi wa maliasili za nchi, haki za watu wenye ulemavu hususan wenye ualbino, pamoja na kuondoa ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mheshimiwa Zainab Katimba (katika) waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa lengo kuu la UPR ni kuboresha hali ya haki za binadamu na kuleta matokeo makubwa kwa watu wote ulimwenguni, huku ikisaidia nchi kutimiza wajibu wake katika mikataba ambayo imeridhia.



Post a Comment

0 Comments