SUAMEDIA

SUA, AFIDA na IFA watoa mafunzo ya mbolea endelevu kwa wanafunzi

 Na: Ngolo Mboje – Morogoro.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Chama cha Maendeleo ya Sekta ya Mbolea Barani Afrika (AFIDA) na Chama cha Kimataifa cha Mbolea (IFA), kimetoa mafunzo maalum kuhusu matumizi endelevu ya mbolea na afya ya udongo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kushirikisha viwanda na makampuni kwenye mafunzo ujuzi.

 

Mkurugenzi Mkuu wa AFIDA, Dkt. Innocent Okuku akizungumza kwenye mafunzo hayo.

Awali akiwakaribisha wageni hao, Rasi wa Ndaki ya Kilimo SUA, Dkt. Nyambilila Amuri, amesema SUA inathamini ushirikiano na taasisi za kimataifa katika kuboresha ubora wa elimu na utafiti. Amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa wanafunzi kupata maarifa ya vitendo yatakayowawezesha kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo.

Dkt. Nyambilila amesema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza ujuzi kwa wahitimu wa Shahada za kilimo na kuongeza uzalishaji wa kilimo endelevu barani Afrika.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa AFIDA, Dkt. Innocent Okuku, amesema lengo la mpango huo ni kusaidia Afrika kujitegemea kwa chakula kwa kuongeza uzalishaji na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa za kilimo kutoka nje ya bara.

Aidha amesema AFIDA inawaleta pamoja wadau wote wa sekta ya mbolea ili kuhakikisha matumizi sahihi na endelevu yanaongeza tija ya mazao.

Dkt. Okuku amebainisha kuwa mafunzo hayo yamelenga wanafunzi wa fani za Kilimo na Mazingira na kwamba katika wiki hii, mafunzo hayo yametolewa kwa wanafunzi wa mwaka wa mwisho katika fani za Ualimu wa kilimo na biolojia, Uhandisi wa Kilimo, Uhandisi wa Umwagiliaji na Rasilimali Maji, kwa lengo la kuwajengea uwezo unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

 Aidha, amesema ushirikiano kati ya vyuo vikuu na sekta binafsi utasaidia kupunguza pengo kati ya elimu ya darasani na uhalisia wa kazi.

 “Afrika bado inatumia kiwango kidogo cha mbolea, wastani wa kilo 20 kwa hekta ikilinganishwa na zaidi ya kilo 100 duniani, hali inayochangia uzalishaji mdogo wa mazao hivyo ni lazima  tuwekeze zaidi katika uzalishaji wa mbolea ndani ya bara pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara kati ya nchi za Afrika” Alisisiiza Dkt. Okuku.

Kwa upande wao, mmoja wa wanafunzi wa SUA, Lilian Benjamin anayesoma Shahada ya Sayansi ya Uhandisi wa Kilimo pamoja na Maranatha Kidava, mwanafunzi wa Shahada ya Uhandisi wa Umwagiliaji na Rasilimali Maji, wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kuongeza uelewa wa vitendo kuhusu matumizi sahihi ya mbolea na umuhimu wa afya ya udongo katika kuongeza uzalishaji wa mazao.

Wamesema maarifa waliyoyapata watayatumia katika taaluma zao na kuyasambaza kwa wakulima katika jamii ili kuongeza tija ya uzalishaji endelevu na kuimarisha usalama wa chakula, huku wakisisitiza kuwa vijana wana nafasi kubwa katika kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya kilimo nchini na barani Afrika kwa ujumla.


                          MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA MAFUNZO HAYO.








Post a Comment

0 Comments