Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Wataalamu
wa afya na mazingira wameendelea kuonesha wasiwasi juu ya kuenea kwa magonjwa
ya malaria na kichocho barani Afrika, wakieleza kuwa bado ni miongoni mwa
changamoto kubwa za kiafya zinazoathiri maendeleo ya jamii hasa kutokana na
kushamiri kwa kilimo cha mpunga kwenye maeneo mengi na kuongeza mazalia ya Mbu
na Konokono wamaoneza magonjwa hayo.
Hayo
yamesemwa na wataafiti kutoka Shule ya London ya Usafi wa Afya na Tiba ya
Magonjwa ya Tropiki Prof. Jo Lines na Dkt. Laura Braun wakati wakifanya
wasilisho lao mbele ya watafiti wa Mradi wa Mpunga Himilivu kwa mabadiliko ya
Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira barani Afrika (CERA) pamoja na Watafiti wa Kituo
cha Kusini mwa Afrika cha Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Kuambukiza (SACIDS) kuhusu
mahusiano ya magonjwa hayo lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kuangalia namna ya kuongeza ushirikiano na kubuni njia za pamoja za kukabiliana
na kuenezwa kwa magonjwa hayo nchini Tanzania.
Akifanya
wasilisho lake Prof. Jo Lines alieleza kuwa pamoja na jitihada mbalimbali
zinazofanyika, ugonjwa wa malaria bado unaathiri kwa kiwango kikubwa bara la
Afrika, na hivyo kuhitaji mikakati madhubuti zaidi ya kudhibiti na hatimaye
kuutokomeza.
“Afrika inabeba zaidi ya asilimia 85 ya
mzigo wa malaria duniani lakini pia unaendelea kusababisha vifo kila dakika, hali inayodhihirisha
uzito wa tatizo hili na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na shirikishi
katika kupambana nao kwani mbu aina ya Anopheles gambiae ndiye
msambazaji hatari zaidi wa malaria barani Afrika nah ii ni kwa sababu mbu huyu ana uwezo mkubwa wa kusambaza vimelea
vya ugonjwa huo kwa ufanisi mkubwa ikilinganishwa na aina nyingine za mbu
wanaopatikana katika maeneo mengine duniani” alifafanua Prof. Lines.
Kutokana
na hali hiyo, amesisitiza kuwa udhibiti wa mbu hawa unapaswa kupewa kipaumbele
kwa kutumia mbinu jumuishi huku akipendekeza matumizi ya vyandarua vyenye dawa,
kunyunyizia viuatilifu, pamoja na kuboresha mazingira ili kupunguza mazalia ya
mbu, hususan katika maeneo yenye maji yaliyotuama.
Katika hatua nyingine, Prof. Jo Lines
aliangazia uhusiano uliopo kati ya malaria na kilimo cha mpunga na kusema kuwa zao
la mpunga linaendelea kukua kwa kasi barani Afrika na hasa katika maeneo ya
karibu na miji, jambo ambalo linaongeza uzalishaji wa chakula lakini pia
linaibua changamoto mpya za kiafya.
Aidha alifafanua kuwa mashamba ya mpunga
yanaweza kuwa mazalia mazuri ya mbu kutokana na uwepo wa maji ya kudumu na muda
mfupi hali hii inaweza kuongeza hatari ya maambukizi ya malaria endapo hatua
stahiki za udhibiti hazitachukuliwa.
Akizungumzia
ugonjwa wa Kichocho (schistosomiasis) Dkt. Laura Braun alieleza kuwa ugonjwa
huo unaendelea kuwa tishio kubwa la afya ya jamii, hasa katika maeneo yenye
vyanzo vya maji yasiyo salama na kubainisha kuwa ugonjwa huo husababishwa na
minyoo aina ya Schistosoma
na unaathiri zaidi ya watu milioni 240 duniani.
Dkt. Braun
alifafanua kuwa maambukizi ya ugonjwa huo hutokea pale mtu anapogusana na maji
yenye konokono walioambukizwa ambao hubeba vimelea vinavyoweza kupenya moja kwa
moja kupitia ngozi ya binadamu na kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwemo
upungufu wa damu na uharibifu wa viungo vya ndani.
“Mazingira ya kilimo cha mpunga yanaweza
kuongeza hatari ya maambukizi ya kichocho kwani maji ya kina kifupi, yenye joto
na yasiyotembea kwa kasi huwa mazuri kwa kuzaliana kwa konokono wanaobeba
vimelea hivyo na kutokana na hali hiyo wakulima wa mpunga huwa katika hatari
kubwa zaidi ya kuambukizwa kutokana na kukaa muda mrefu ndani ya maji wakati wa
shughuli za kilimo” alibainisha Dkt. Braun.
Mtafiti
huyo amesisitiza umuhimu wa wakulima kuchukua hatua za kinga, ikiwa ni pamoja
na kuvaa vifaa vya kujikinga kama buti, kuboresha usimamizi wa maji mashambani,
na kutoa elimu kwa jamii kuhusu njia za maambukizi.
Sambamba
na hilo alieleza kuwa ushirikiano kati ya sekta ya afya na kilimo ni muhimu ili
kuhakikisha kuwa uzalishaji wa chakula unaenda sambamba na ulinzi wa afya za
wananchi kwa kufanya kilimo rafiki kwa binadamu na kinachozuia kuzaliana kwa
konokono hao pamoja na mbu hao wanaoeneza ugonjwa wa Maralia.
Awali
akizungumzia lengo la ziara hiyo ya watafiti nchini Mtafiti Mkuu wa Mradi wa
Mpunga Himilivu kwa mabadiliko ya Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira barani
Afrika (CERA) Prof. Suzana Nchimbi Msolla amesema watafiti hao wanatafuta njia
rafiki ambayo inaweza kutumika kwenye mashamba hayo ya mpunga kuzuia kuzaliana
kwa vimelea vya magonjwa hayo kwa kufuga samaki na bata ambao watakula mayai na
vuluilui vya Mbu na Konokono na kupunguza kuzaliana na kutunza afya ya binadamu
pamoja na kuongeza kipato kwa wakulima.
“Wamekuja
baada ya kuona kuwa sisi kama mradi tunafanya utafiti kwenye zao la mpunga kwa
muda mrefu hivyo wakataka kutushirikisha kuhusu utafiti wao na kujadiliana
kuona uwezekano wa matumizi ya njia wanazopendekeza kama zitafaa kwa mazingira
ya Tanzania hasa baada ya kuona kuwa njia kama hizo zimeweza kufanya kazi
kwenye nchi zingine kama vile China,Mashariki kwa ulaya na Asia ya kati”
Alieleza Prof. Msolla.
Prof.
Msolla amesema wataalamu bado wanasisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kinga
kama vile kuvaa vifaa vya kujikinga (boots), kuboresha usimamizi wa maji
mashambani, pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu njia za maambukizi kwani
hatua hizp zinaweza kusaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa athari za ugonjwa huu
katika jamii zinazotegemea kilimo cha mpunga.
![]() |
| Mkurugenzi wa Kituo cha Kusini mwa Afrika cha Ufuatiliaji wa Magonjwa ya Kuambukiza (SACIDS) Prof. Gerald Misinzo akieleza uzoefu wake kwenye magonjwa ya kuambukiza kupitia mbinu ya Afya moja. |
![]() |
| Mtafiti Mbobevu kwenye Ufugaji wa viumbe maji kutoka Idara ya Sayansi ya Wanyama na Viumbebaji ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Dkt. Renalda Mnubi akieleza jambo wakati wa mjadala huo. |
![]() |
| Watafiti hao wakichua sampuli kwaajili ya kupeleka maabara za SUA kuangalia uwepo wa vimelea kwenye eneo la shamba la majaribio ya kilimo cha mpunga. |














0 Comments