Na: Vumilia Kondo
Chuo
Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) kimepiga hatua nyingine kubwa katika kuandaa
wataalamu wa kilimo cha kisasa baada ya kuendesha mafunzo ya vitendo ya
teknolojia ya ndege nyuki (droni) kwa wanafunzi wote wanaosomea fani mbalimbali
za kilimo na ufugaji.
![]() |
| Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda akizungumza na wanafunzi (hawako pichani) kushoto ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Utawala na Fedha Prof. Amandus Muhairwa |
Mafunzo
hayo yamefanyika kwa lengo la kuwapa vijana ujuzi wa jinsi ndege nyuki zinavyoweza
kutumika kupulizia viuadudu, kufanya tathmini ya afya ya mazao, na ramani za
kidijitali za mashamba.
Makamu
Mkuu wa Chuo, Profesa Raphael Chibunda, akizungumzia uzito wa mafunzo hayo,
amebainisha kuwa chuo kimefanya maamuzi ya makusudi kuwekeza kwenye teknolojia
hiyo ili kuendana na dira ya Serikali ya Awamu ya Sita.
![]() |
| Wanafunzi wakishiriki mafunzo ya kurusha ndege nyuki |
"Tumetenga
bajeti kwa ajili ya kukuboresha jinsi tunavyofundisha wanafunzi wetu. Sisi kama
wafundishaji hatuwezi kubaki nyuma, yaani tukaacha wahitimu wetu wakaenda kuona
hivi vitu wanapokuwa wamemaliza chuo. Tumejipanga ili wawe waajiriwa bora, lakini
sehemu kubwa wawe na ujuzi wa kwenda kujiajiri," amesema Profesa Chibunda.
Naye
Rasi wa Ndaki ya Kilimo, Dokta Nyambilila Amuri akifafanua kiufundi kuhusu
umuhimu wa mafunzo hayo, amesema matumizi ya droni ni sehemu ya utekelezaji wa
mitahala mipya inayolenga kilimo cha uhakika (Precision Agriculture).
![]() |
| Rasi wa Ndaki ya Kilimo, Dokta Nyambilila Amuri akizungumza na mwandishi wa SUA Media |
"Matumizi
ya droni yanaleta kilimo cha uhakika (precision agriculture). Tutaweza kutumia
mbolea na viuatilifu kwa kiwango sahihi na kwa eneo sahihi, jambo linaloongeza
tija na ufanisi wa pembejeo, huku tukikabiliana na changamoto za mabadiliko ya
tabianchi kwa kufanya kilimo kiwe rafiki kwa mazingira."
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya
Agri Mazao Mohamedi Salimu, ameeleza kuwa ushirikiano wao na SUA unalenga
kuwapa wanafunzi uzoefu wa vitendo kutoka sokoni.
![]() |
| Ndege nyuki ikiwa angani |
Amebainisha kuwa droni zina uwezo wa kufanya
kazi kubwa kwa muda mfupi, jambo ambalo ni mkombozi kwa mkulima katika
kupunguza gharama za vibarua na dawa.
Wanafunzi
walioshiriki mafunzo hayo akiwemo Elizabeth
Salim anayesomea uzalishaji na usimamizi wa mazao wameeleza namna
teknolojia hiyo inavyobadilisha mtazamo wao wa kilimo.
"Zamani
tulikuwa tunaangalia matatizo ya shambani kwa macho, lakini sasa hivi droni
inatusaidia kuditekti (detect) matatizo na kurahisisha kazi ya kupulizia magugu
na wadudu kwenye mahindi, jambo ambalo linapunguza gharama za uzalishaji."Amesema
Elizabeth
![]() |
Naye
mwanafunzi Frankie Daudi ameongeza kuwa droni inasaidia kufanya 'mapping' ya
eneo lote la shamba kwa muda mfupi na kwa usahihi wa hali ya juu ikilinganishwa
na njia za kawaida.
Tukio
hili linaashiria mwanzo wa msimu mpya wa mafunzo ambapo SUA imejipanga
kuhakikisha teknolojia inakuwa nguzo kuu ya kilimo, ikiendana na kaulimbiu ya
chuo hicho kuwa "Ardhi ni Hazina."





0 Comments