SUAMEDIA

Serikali na wadau waombwa kumwezesha Mwanaume kwa naufaa ya Jamii na Taifa

 Na: Adam Maruma – Morogoro.

Serikali pamoja na wa wadau wa maendeleo wametakiwa kumwezesha mwanaume kwenye harakati mbalimbali za kiuchumi na kijamii  ili aweze kuwa nguvu na ushawishi katika jamii itakayomjengea kujiamini na kuanzisha familia atakayoisimamia kwa faida ya jamii na taifa kwa ujumla.

Baadhi ya washiriki wa siku ya mwanaume Duniani wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya kuhitimishwa kwa Kongamano hio mjini Morogoro.

Wito huo umetolewa na Mhadhiri mwandamizi wa masuala ya Jinsia , sayansi ya jamii  na maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Rasel Madaha katika maadhimisho ya siku ya mwanaume wa kitanzania iliyofanyika katika ukumbi wa Soko la Chief Kingalu uliopo Manispaa ya Morogoro.

Prof. Madaha amesema kuwa  harakati mbali mbali zimekuwa zikimlenga zaidi mwanamke na kumsahau mwanaume ambae wakati mwingine amekuwa na changamoto nyingi zaidi.

Mhadhiri mwandamizi wa masuala ya Jinsia , sayansi ya jamii  na maendeleo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA Prof. Rasel Madaha akizungumza na Waandishi wa habari nje ya Kongamano hilo.

Aidha ameongeza kuwa kutokana na mabadiliko ya kiuchumi nchini na duniani kote wanaume kama walezi na wasimamizi wa familia wamekuwa na changamoto mbali mbali za kijamii na kiuchumi na hivyo kushindwa kuanzisha na kusimamia familia kama ilivyo katika miaka ya nyuma.

Mhadhiri huyo mwandamizi amesema  kuna kila sababu ya Serikali na wadau mbali mbali,kumwezesha katika harakati mbali mbali za kiuchumi, na kijamii ili waweze kuinuka kuichumi.

Msomi huyo wa masuala ya usawa wa kijinsia na maendeleo amesema jamii imakuwa na dhana ya kumuona mwanaume kama mtu asiyehitaji msaada wowote,hali inayowapelekea wanaume wengi kujikuta wakishindwa kupata misaada mbali mbali ya kiuchumi na hivyo kubaki na changamoto ambayo huwapelekea wanaume wengi kupata msongo wa mawazo na kufanya matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wenza na watoto wao au wakati mwingine kujiua wao wenyewe.

Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Cha Mipango Dodoma Christina Mandara, amesema siku ya mwanaume wa Kitanzania, ni siku muhimu ili kukumbusha na kuifundisha jamii kuhusu kazi, majukumu na thamani ya mwanaume kwenye jamii na familia kwa taifa kwa ujumla.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Cha Mipango Dodoma Christina Mandara, akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya Kongamano hilo.


Ameongeza kuwa mwanaume wa sasa bila kujali umri wao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi kutokana  na mabadiliko ya kiteknolojia na fursa za kiuchumi kwa wanaume na wanawake hali inayopelekea changamoto mbalimbali za kimalezi.

Amefafanua kuwa hali hiyo inayopelekea mabadiliko ya kimfumo wa kimalezi na ukuaji wa mitandao ya kijamii pia imekuwa na changamoto zaidi kwenye eneo la malezi ya kwa kufanya jamii kupata mafunzo yasiyo mazuri kwa jamii kupitia mitandao hiyo.

Nae Mhadhiri mwingine Dkt. Jonas Gervas kutoka Chuo cha Ardhi katika wasilisho lake amewaomba wanaume kugeuza changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii kuwa fursa za ajira akitolea mfamo wa namna taka zinavyoweza kuwa chanzo kizuri cha ajira kwa kuzigeuza kuwa malighafi ya kutengeneza bidhaa mbali mbali kama mkaa na mbolea kwa matumizi ya kilimo.

 Mhadhiri kutoka Chuo cha Kikuu cha Ardhi Dkt. Jonas Gervas akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa habari mara baada ya kongamano hilo.

Amesema kutokana na ongezeko la watu kumekuwa pia na ongezeko la uzalishaji wa taka katika miji na majiji yenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini kama Dar Es Saalaam hivyo tafiti zinaonesha kuwa uhudumiaji wa taka hizo umekuwa changamoto kwa halmashauri na majiji hivyo changamoto hiyo inaweza kuwa chanzo cha ajira kwa wanaume kutokana na kuwa kumekuwa na viwanda ambavyo vinafanya urejeshelezaji wa taka hizo kwa matumizi mingine.

Siku ya Mwanaume wa Kitanzania imeadhimishwa kwa mwaka wa 3 tangu kuasisiwa kwake 2024 ambapo kwa mwaka huu imeboreshwa zaidi kwa kuwa na usalishaji wa mada mbali mbali za kitaaluma kutoka vyuo vikuu nchini kama Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, SUA, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Chuo cha Mipango Dodoma, Chuo Kikuu Ardhi, pamoja na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, huku washiriki wakijadili mada mbali mbali na kubadilishana na uzoefu na kuongeza udadisi wa masuala ya usawa wa kijinsia ili viweze kwenda pamoja na maendeleo jumuishi.

PICHA KATIKA MATUKIO NI BAADHI YA WASHIRIKI WA KONGAMANO HILO WAKIFUATAILI MADA ZINAZOWASILISHWA.








Post a Comment

0 Comments