Na: Vumilia Kondo
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kimeendelea kudhihirisha kuwa kitovu cha elimu ya juu ya kilimo barani Afrika
baada ya kupokea ujumbe wa watafiti na wasomi sita kutoka Chuo Kikuu cha
Sayansi na Teknolojia ya Kilimo cha Marondera (MUAST) cha nchini Zimbabwe.
Ujumbe huo ukiongozwa na Dkt. Witness Kozanayi, ambaye ni Mtafiti Mkuu wa mradi wa RAENS, umewasili chuoni hapo kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kubadilishana uzoefu, kujifunza mifumo ya kisasa ya ufundishaji, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda ndani ya SADC.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt.
Kozanayi amebainisha kuwa uamuzi wa kuja SUA haukuwa wa kubahatisha.
"Tulitafuta mshirika wa kimkakati sehemu
mbalimbali, lakini tulivutiwa na historia ndefu ya SUA katika utafiti na
ufundishaji wa kilimo kwa ujumla, na hususan katika nyanja ya
Kilimo-Ekolojia," amesema Dkt. Kozanayi.
Ameongeza kuwa kupitia ushirikiano wao na Prof. Dismas Mwaseba wa SUA katika mradi wa RAENS, wamegundua kuwa SUA ina utajiri mkubwa wa programu za masomo (degree programs) na mitandao ya kikanda ambayo MUAST, ikiwa ni chuo kinachochipukia nchini Zimbabwe, kinatamani kujifunza namna ya kuiratibu.
Katika
ziara hiyo, ujumbe huo umetembelea maeneo mbalimbali muhimu yanayoakisi
maendeleo ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ikiwemo Hospitali ya
Wanyama, vitalu nyumba pamoja na maeneo ya ufugaji samaki, ambapo Dkt. Kozanayi
amevutiwa na matumizi ya teknolojia za kisasa katika uzalishaji wa mazao na
samaki zinazoweza kuwasaidia wakulima wadogo kuongeza tija; aidha, Jengo la
Mafunzo la Dkt. Samia Suluhu Hassan limewavutia wageni hao kama mfano bora wa
uwekezaji katika miundombinu ya elimu ya juu.
Dkt. Kozanayi amesisitiza kuwa MUAST inatekeleza mfumo wa "Education 5.0" nchini Zimbabwe, ambao unahimiza vyuo vikuu kutofanya kazi ya kufundisha na kufanya utafiti pekee, bali kujikita katika ubunifu, viwanda, na huduma kwa jamii.
"Tumejifunza mengi kuhusu namna
SUA inavyofanya tafiti zinazoongozwa na wakulima wenyewe na jinsi ya
kubadilisha mawazo ya kitaaluma kuwa bidhaa za kibiashara, hili ni eneo ambalo
SUA mko vizuri sana," alisisitiza Dkt. Kozanayi.
Mbali na mradi wa RAENS, ziara hii
inafungua milango ya mabadilishano ya wanafunzi wa shahada za juu.
Dkt.
Kozanayi amesema anatarajia kuona wanafunzi kutoka Zimbabwe wakija SUA na wale
wa Tanzania wakienda Zimbabwe ili “kuachana na mazoea waliyojengeka nayo” na
kujifunza mbinu mpya zitakazochangia maendeleo ya kanda ya Kusini na Mashariki
mwa Afrika.




0 Comments