Na: Farida Mkongwe
Wanawake wa Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na wafanyakazi wengine wa chuo hicho
wamefanya matendo ya huruma kwa kutoa misaada ya vitu mbalimbali ikiwemo nguo,
sukari, unga, sabuni na mafuta kwa wahitaji wa Kata ya Kauzeni iliyopo Manispaa ya Morogoro pamoja na Kituo
cha Watoto cha Sarafina kilichopo katika kata hiyo ikiwa ni sehemu ya
maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, kwa lengo la kuonesha upendo na mshikamano
kwa jamii.
Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake wa Chama cha Wafanyakazi RAAWU Tawi la SUA ambaye pia ni mratibu wa shughuli hiyo, Bi. Enessa Mlay, amesema wanawake wa SUA wameona umuhimu wa kuadhimisha siku hiyo kwa vitendo kwa kuwafikia wananchi wanaohitaji msaada ili kuonesha mshikamano kwa jamii kwa kufanya matendo ya huruma.
“Kipindi hiki ni cha mfungo wa mwezi
mtukufu wa Ramadhani na Kwaresima, ambacho tunahimizwa kufanya matendo mema na
kusaidiana katika jamii, lengo letu kubwa ni kuacha alama ya upendo na
kuwakumbusha wananchi kuwa SUA ipo karibu nao na inaendelea kujali ustawi wa
jamii inayowazunguka”, amesema Bi. Mlay.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kauzeni, Vicent Zakaria Katabi, amewashukuru wanawake na wafanyakazi wa SUA kwa moyo wao wa kujitoa kusaidia jamii na kwamba msaada huo umeleta faraja kubwa kwa wananchi wa Kauzeni na ni mfano mzuri wa kuigwa na wadau wengine, huku akisisitiza kuwa kufanya matendo ya huruma ni ibada na kunaleta faraja kwa wale wanaohitaji msaada.
Naye Mratibu wa tawi la Shirika
la SAFINA Street Network Morogoro, Amani Evarist Kumba, amewashukuru wanawake
wa SUA kwa msaada wao na kuwataka wawe mabalozi wazuri wa kuitangaza taasisi
hiyo inayofanya kazi ya kuwasaidia
watoto na vijana waliowahi kuishi na kufanya kazi mitaani ili wadau zaidi
waweze kujitokeza na kuwawezesha katika mahitaji mbalimbali.
Amesema kwa sasa shirika hilo ambalo lina matawi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Iringa, Singida na Dodoma, kwa mwaka huu linawahudumia watoto 40 mkoani Morogoro kwa kuwapatia huduma za chakula, mavazi, matibabu na elimu kuanzia shule ya msingi hadi chuo.
Kwa upande wake, mkazi wa Kata
ya Kauzeni, Aziza Ally Kilongola, ametoa shukrani kwa wanawake wa SUA kwa
msaada walioutoa akisema umeleta faraja kwa wanufaika na jamii kwa ujumla.
Amesema jamii ya Kauzeni inathamini mchango huo na kuwataka wadau wengine kuendelea kujitokeza kusaidia wahitaji ili kuimarisha mshikamano na ustawi wa jamii.
.jpeg)






0 Comments