SUAMEDIA

Waziri Mkuu kuweka jiwe la msingi la majengo ya taaluma na bweni SUA – Kampasi ya Mizengo Pinda

 Na: Asifiwe Mbembela

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kikili (SUA) kinatarajia kuandika historia mpya kufuatia kufanyika kwa Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Taaluma na Bweni katika Kampasi ya Mizengo Pinda, itakayofanyika siku ya Jumamosi, tarehe 14 Machi, 2026.

Mgeni Rasmi, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye anatarajiwa kuweka jiwe la msingi kuashiria mwanzo wa utekelezaji wa mradi huo muhimu wa kimkakati.

Ujenzi wa majengo hayo unatekelezwa kwa ufadhili wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaolenga kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia vyuo vikuu nchini.

Mradi huu pia utaboresha mazingira ya malazi kwa wanafunzi na hivyo kuongeza ufanisi wa shughuli za kitaaluma pamoja na ustawi wa wanachuo kwa ujumla.

Kupitia mradi huu, Chuo kitaongeza uwezo wa kuhudumia wanafunzi wengi zaidi sambamba na kuboresha ubora wa mazingira ya kujifunzia, jambo litakalochochea maendeleo ya taaluma, tafiti na ubunifu.

Maboresho haya ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha sekta ya elimu ya juu ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na ushindani katika soko la ajira.

Chuo kinatoa pongezi za dhati kwa Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya elimu ya juu na miundombinu yake, uwekezaji huu unaonesha dhamira thabiti ya Serikali ya kuhakikisha vyuo vikuu vinakuwa na mazingira bora yanayowezesha utoaji wa elimu yenye ubora wa kimataifa.




Post a Comment

0 Comments