SUAMEDIA

Tanzania Kinara Afrika kwa Teknolojia ya DNA katika Kilimo

 Na: Calvin Gwabara – Dar es salaam.

Tanzania imeibuka kuwa kinara barani Afrika katika matumizi ya teknolojia ya vinasaba (DNA) kukabiliana na wadudu na magonjwa ya mazao.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru akionesha kifaa hicho cha kisasa cha utambuzi wa magonjwa na wadudu papohapo.

Akizungumza katika mkutano wa wadau wa bioteknolojia (BST) Prof.  Joseph Canisius Ndunguru, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA), amesema hatua hiyo ni mapinduzi ya kisayansi yanayobadilisha usimamizi wa afya ya mimea na usalama wa chakula nchini.

“TPHPA ilianzishwa chini ya Sheria ya Afya ya Mimea Na. 4 ya mwaka 2020 kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa afya ya mimea na viuatilifu na lengo lilikuwa kuunda mfumo madhubuti wa kisheria na kisayansi unaolinda wakulima, walaji na maslahi ya biashara ya kimataifa.Alibainisha Prof. Ndunguru.

Amesema miongoni mwa wadudu hatari ni viwavijeshi vamizi anayejulikana kama funza wa majani ya Mahindi (Fall Armyworm), ambaye amesababisha hasara kubwa ya mazao barani Afrika ambapo katika baadhi ya maeneo, wakulima wamepoteza hadi asilimia 60 ya mavuno.

Alieleza kuwa wakulima wengi hulazimika kunyunyiza viuatilifu mara kwa mara na kuchanganya kemikali kadhaa lakini unyunyiziaji holela si suluhisho na unaongeza hatari za kiafya na kuharibu mazingira.

Prof. Ndunguru amebainisha kuwa Ili kukabiliana na changamoto hiyo, TPHPA imeanza kutumia vifaa vya kubebeka vya uchunguzi wa DNA vinavyoweza kubaini aina halisi ya mdudu au kisababishi cha ugonjwa shambani.

 “Tanzania imekuwa nchi ya kwanza duniani kutumia teknolojia hii katika sekta ya kilimo kwa kiwango cha kitaifa,” alisema Prof. Ndunguru.

Aidha Mkurugenzi huyo mkuu wa TPHPA amesema Teknolojia hiyo ilithibitika wakati wa uvamizi wa nzige katika Wilaya ya Mpwapwa. Uchunguzi wa DNA ulithibitisha kuwa walikuwa Anacridium incisum badala ya nzige wekundu waliokuwa wakihofiwa na hivyo uUtambuzi sahihi uliwezesha kutumia dawa maalumu na kudhibiti uvamizi huo kwa mafanikio.

Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru akiwa kwenye moja ya mashamba na watalamu wake wakitumia kifaa hicho kutambua visumbufu vya mazao ya wakulima vijijini kwenye maeneo ya Kilolo Mkoani Iringa.

Akieleza eneo lingine ambalo vifaa hivyo vimetumika amesema ni wilaya ya Kilolo, uchunguzi wa kina ulibaini uwepo wa vimelea mbalimbali vilivyoathiri nyanya na vitunguu kwa wakati mmoja na kugundua kuwa mazao yalikuwa yanashambuliwa na mtandao wa magonjwa unaohusisha fangasi, bakteria na virusi kwa pamoja.

“Teknolojia hii pia imeimarisha biashara ya kimataifa kwani baada ya Umoja wa Ulaya kuhitaji uthibitisho kuwa Tanzania haina bakteria hatari wa Xylella, TPHPA ilifanya maelfu ya vipimo vya maabara, na hivyo kutokana na ripoti yetu ya kisayansi, Tanzania iliendelea kuruhusiwa kufanya biashara na EU,” alieleza Mkurugenzi huyo Mkuu wa TPHPA Prof. Ndunguru.

Mbali na hilo, TPHPA imewekeza katika maabara za kisasa zenye uwezo wa kuchambua sampuli 2,000 za viuatilifu kwa wiki kwani dhibiti unaotegemea sayansi unahakikisha wakulima wanapata viuatilifu salama na sahihi kwani dhamira ya TPHPA ni kujenga mfumo wa kilimo endelevu na himilivu. Bioteknolojia si anasa bali ni hitaji la msingi kwa mustakabali wa usalama wa chakula.

 

Post a Comment

0 Comments