Na: Calvin Gwabara – Dar es salaam.
Serikali imetangaza kuwa
bioteknolojia itakuwa mhimili mkuu wa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo
2050, kwa lengo la kuongeza usalama wa chakula, ajira na ushindani wa uchumi wa
Tanzania.
Akizungumza Dar es Salaam wakati wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Bioteknolojia Tanzania (BST),Naibu katibu Mkuu wizara ya Kilimo anayeshughulikia maendeleao ya mazao na usala wa chakula Prof. Peter Msoffe kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo alisema teknolojia hiyo itawezesha uzalishaji wa mazao yanayostahimili mabadiliko ya tabianchi, kuongeza tija mashambani na kusaidia mapinduzi ya viwanda na afya.
“Bioteknolojia si chaguo tena bali
ni hitaji la lazima kama tunataka Tanzania iwe na usalama wa chakula, ajira kwa
vijana na uchumi wa kisasa unaotegemea sayansi, teknolojia na ubunifu” Alisema
Prof. Msoffe.
Alisema bioteknolojia itasaidia
pia sekta ya afya kwa kuzalisha chanjo, tiba za jeni na vipimo vya vinasaba
vitakavyotambua magonjwa mapema, pamoja na kudhibiti malaria kupitia teknolojia
za kisasa za kudhibiti mbu.
Aliongeza kuwa Serikali pia
inaendelea kufanya maboresho ya sera na sheria ili kuhakikisha matumizi ya
teknolojia hii yanafanyika kwa usalama bila kuathiri binadamu, wanyama na
mazingira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
BST Prof. Peter Msolla alisema Tanzania haina budi kuwekeza katika utafiti wa
bioteknolojia katika mazao muhimu kama mahindi, mpunga, mihogo na migomba ili
kukabiliana na changamoto za uzalishaji.
Alisema bila utafiti, nchi
haiwezi kupata faida kamili za teknolojia hiyo wala kuwajibu wadau wanaohoji
usalama wake.
“Bila kuwekeza katika utafiti wa
bioteknolojia, Tanzania itaendelea kulima kwa mazoea badala ya kutumia sayansi na
hilo litatuacha nyuma katika ushindani wa chakula, biashara na maendeleo.”Alisisitiza
Prof. Msolla.
BST pia imekuwa ikielimisha umma kuhusu bioteknolojia ili
kuondoa hofu na dhana potofu, huku ikisisitiza kuwa teknolojia hii inaweza
kubadili kabisa kilimo na uchumi wa nchi iwapo itaungwa mkono kwa sera rafiki,
uwekezaji na uelewa wa jamii.
HABARI PICHA WAKATI WA MKUTANO HUO.





0 Comments