SUAMEDIA

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinafanya mageuzi makubwa kupitia mradi wa HEET.

 Na: Ngolo Mboje   - Morogoro.                                     

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kinapitia mageuzi makubwa kwa kuboresha miundombinu ya kufunindishia na kujifunzia na hivyo kupelekea kuongeza uwezo wake wa kudahili wanafunzi wengi zaidi baada ya kukamilika kwa majengo makubwa na ya kisasa yanayojengwa chini ya Mradi wa HEET.

Moja kati ya Sehemu ya majengo yanayojengwa kupitia mradi wa HEET kwenye Chuo Kikuu kikuu cha Sokoine.

Akiwa katika ziara ya ukaguzi wa majengo hayo kwenye Kampasi ya Mazimbu  Mkoani Morogoro, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango Utawala na Fedha Prof. Amandus Muhairwa amesema kuwa  mradi umeongeza ubora na ufanisi wa mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kupitia ufadhili wa mkopo wa Benki ya Dunia wa masharti nafuu kupitia Serikali ya Tanzania umewezesha kujenga na kukarabati majengo ya kisasa yanayoongeza uwezo wa kupokea wanafunzi wengi zaidi hatua ambayo inaimarisha nafasi ya SUA kuwa Kitovu cha Elimu ya Kilimo na Sayansi shirikishi.

“Sisi kama chuo tumehakikisha kuwa ujenzi na matumizi ya miundombinu mipya yanazingatia usalama wa wafanyakazi, ustawi wa jamii zinazozunguka na hifadhi ya mazingira lakini pia inaleta taswira ya chuo kinachojali si tu elimu, bali pia uwajibikaji wa kijamii na uendelevu wa mazingira kwa wanafunzi na walimu, ikiwa pia ni fursa ya kujifunza katika mazingira salama, yenye uwazi na yanayoheshimu viwango vya kimataifa” alibainisha Prof.Muhairwa.

Naibu huyo wa makamunwa Mkuu wa Chuo amesema mradi huo utaimarisha uwezo wa SUA katika mafunzo, utafiti na ubunifu na hivyo HEET kuchangia moja kwa moja katika ajenda ya kitaifa ya mageuzi ya kiuchumi.

Baadhi ya viongozi wa Menejimenti ya Chuo wakipata maelezo kwa wakandarasi juu ya maendeleo ya ujenzi wa majengo.

Amesema kupitia maboresho hayo makubwa yatasaidia wataalamu wanaohitimu kutoka SUA watakuwa na ujuzi na maarifa ya kisasa ya kilimo na sayansi zinazohusiana hivyo kusaidia kuongeza tija kupunguza umasikini na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

“Naweza kusema kuwa maneno mengine mradi huu unaiwezesha SUA kuwa daraja kati ya Elimu ya juu na maendeleo ya Taifa, na matokeo yake yataendelea kuonekana kwa vizazi vijavyo” Alisisitiza Prof. Muhairwa.

Utekelezaji wa Elimu ya Juu na Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya elimu nchini hususani elimu ya juu nchini kupitia maboresho ya miundombinu, kuzingatia viwango vya usalama na uendelevu, pamoja na kuimarisha ubora wa mafunzo na utafiti kwa msingi imara wa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Post a Comment

0 Comments