SUAMEDIA

SUA yaadhimisha Siku ya Wanawake kwa kuhimiza matumizi ya fursa za mafunzo

 Na: Adam Maruma

Wanawake wametakiwa kutumia kikamilifu fursa za masomo na mafunzo zinazotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kujijengea uwezo, kuongeza ujuzi na kuimarisha ushiriki wao katika maendeleo ya jamii.

Wito huo umetolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Amandus Muhairwa, wakati wa hafla ya kuwapongeza wanawake wa chuo hicho katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kwenye ukumbi wa SUA uliopo Nanenane mjini Morogoro.

Prof. Muhairwa amesema kuwa SUA ina mfumo thabiti wa kulinda wanawake na wasichana pamoja na kutekeleza mpango mkakati wa usawa wa kijinsia, hali inayochangia kuwepo kwa mazingira salama na yenye utulivu yanayowezesha wanawake kufikia malengo yao ya kitaaluma na kiutendaji.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Makamu Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo upande wa Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu, Prof. Maulid Mwatawala, amesema kuwa katika uongozi wa Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Raphael Chibunda, wanawake wameendelea kupata nafasi zaidi za uongozi chuoni huku wanafunzi wa kike wakionesha kufanya vizuri kitaaluma.

Prof. Mwatawala amesema kwa sasa chuo kimefikia asilimia 43 katika kuelekea lengo la usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50. Aidha, amewapongeza wanawake kwa juhudi zao katika kazi na mchango wao katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Ameongeza kuwa chuo kina utaratibu mzuri wa kushughulikia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia na kuwahimiza wanawake kutumia kikamilifu fursa za masomo ili kujiendeleza zaidi kitaaluma.

Kwa upande wao, Mwenyekiti wa RAAWU tawi la SUA, Bw. Faraja Kamendu, na Mwenyekiti wa THTU tawi la SUA, Bw. Nickson Mkilamwene, wamesema kuwa kuwapa wanawake nafasi katika ajira na uongozi kunachochea ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi mbalimbali. Viongozi hao pia wamewahamasisha wanawake kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya chuo na kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kulinda maslahi yao ya kikazi na kitaaluma.

Akisoma hotuba kwa niaba ya wanawake wa chuo hicho, Bi. Farida Mkongwe ameishukuru menejimenti ya chuo kwa kuendelea kutoa fursa za mafunzo kwa wanawake, akisema hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ujuzi, uwezo na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.

Ameongeza kuwa utoaji wa mafunzo kwa watumishi unazingatia mipango na bajeti ya chuo, huku akiiomba menejimenti kuendelea kupanua wigo wa fursa hizo ili kuwajengea wanawake uwezo zaidi katika nyanja mbalimbali za kitaaluma na kiutendaji.




Post a Comment

0 Comments