Na: Adam Maruma – Morogoro.
Mkuu wa koa wa Morogoro Mhe.Adam
Malima amesema wanawake wana mchango mkubwa na wa moja kwa moja katika
maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla ndio maana Tanzania imekuwa mfano barani
Afrika katika kuhimiza ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo na
uongozi.
![]() |
| Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Malima akizungumza kwenye siku ya wanawake kimkoa Mkoani Morogoro. |
Mhe. Malima ameyasema hayo wakiatai
akitoa hobutba yake kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika kimkoa
katika Tarafa ya Mikese, Kata ya Mikese, Kijiji cha Fulwe mkoani Morogoro.
Aidha alikumbusha kuwa katika
historia kulikuwa na nyakati ambapo maadhimisho ya Siku ya Wanawake hayakuweza
kufanyika katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Morogoro na nchini kwa ujumla japo
kuwa mapambano ya haki za wanawake yamekuwepo kwa muda mrefu duniani.
Alitoa mfano wa nchi
zilizoendelea kama Marekani, ambapo wanawake hawakuruhusiwa kupiga kura hadi
mwaka 1920, na kuongeza kuwa kabla ya hapo kulikuwa na changamoto za ubaguzi wa
rangi na ajira, na wanawake walikuwa wakilipwa mishahara midogo ikilinganishwa
na wanaume.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alisema
hatua ya wanawake kushika nafasi mbalimbali za uongozi nchini ni mafanikio
makubwa kwa taifa, na kukumbusha kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro alikuwa Anna Abdallah katika miaka ya 1970.
Hata hivyo, Malima alisema bado
kuna changamoto ya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii, ikiwemo visa vya
wanafunzi wa kike kupata ujauzito wakiwa shuleni na hivyo kutumia nafasi hiyo
kuwataka maafisa Maendeleo ya jamii katika Mkoa wa Morogoro, pamoja na Mahakama
na madawati ya jinsia, kutokuwa na huruma katika kushughulikia kesi za aina
hiyo pindi zinapowasilishwa mbele yao.
Pia alitoa onyo kwa wazazi
wanaomaliza kesi za ukatili wa kijinsia kimya kimya majumbani bila kuripoti
katika vyombo vya sharia kwani vitendo hivyo vinachangia kuendeleza tatizo hilo
na kukatiza ndoto za mabinti wengi na hivyo kuwahakikishia kuwa hatakuwa na
huruma kwa kiongozi yeyote katika Mkoa wa Morogoro atakayeshindwa kushughulikia
kesi hizo kwa mujibu wa sheria.
Malima aliwataka viongozi
kuelewa na kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 ili kusaidia
kufikia malengo ya maendeleo ya taifa na kuwa nchi zinazokandamiza haki za
wanawake haziwezi kupiga hatua za maendeleo.
Maadhimisho hayo hufanyika kila
tarehe 8 March ulimwenguni kote, na kwa mwaka huu katika mkoa wa Morogoro yamehudhuriwa na
viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo na wananchi, yakilenga kuendelea
kuhamasisha usawa wa kijinsia na kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo
ya jamii.
MATUKIO KATIKA PICHA SIKU YA WANAWAKE MOROGORO.








0 Comments