SUAMEDIA

Studio mpya za SUA kuimarisha uzalishaji wa vipindi vya redio na televisheni

 Na: Ngolo Mboje

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, amesema kuwa studio mpya za chuo hicho ni nyenzo muhimu katika uzalishaji wa vipindi vya redio, televisheni na maudhui ya mitandao ya kijamii vinavyoweza kusaidia kuonesha mchango wa chuo katika maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo, misitu na sayansi.

Prof. Chibunda ameyasema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa Kitengo cha Mawasiliano na Masomo baada ya kutembelea studio za SUA Media zilizopo chini ya kitengo hicho katika Kampasi ya Edward Moringe, mkoani Morogoro.

Amesema Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) imetoa msaada wa kuboresha studio hizo kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa vipindi vinavyolenga sekta ya kilimo pamoja na kuitangaza SUA kwa jamii.

Aidha, Profesa Chibunda ametoa wito kwa wanahabari wa SUA Media na watumishi wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko kujipanga vizuri katika uzalishaji wa vipindi mbalimbali, kukifahamu chuo kwa undani pamoja na kuhakikisha wanatunza vifaa vya studio ili viweze kutumika kwa ufanisi na kwa muda mrefu.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko cha SUA, Bi. Suzana Mgobeko, ameishukuru Menejimenti ya chuo kupitia mradi wa HEET kwa kuboresha studio hizo na kuahidi kuwa kitengo hicho kitaendelea kuzalisha vipindi bora vya redio, televisheni na mitandao ya kijamii vitakavyochangia kuitangaza SUA na kuimarisha maendeleo ya sekta ya kilimo.


Post a Comment

0 Comments