SUAMEDIA

SUA yatoa vipimo bure vya afya kwa Wanawake

 Na: Ngolo Mboje – Morogoro.

Katika kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimetoa fursa ya  elimu ya afya ya magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza na huduma ya vipimo bure  bila malipo  kwa wanawake wa chuo hicho kwa lengo la kupata uewelewa kuhusu njia za kujikinga na magonjwa mbalimbali.

Baadhi ya Wanawake kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA wakiwa kwenye picha ya pamoja na wawezeshaji kwenye kongamano hilo.

 Akifungua kongamano la wanawake Prof: Faith Philemon Mabiki kutoka Ndaki ya Sayansi Asilia na Tumizi (CoNAs) kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) lililofanyika machi 4, 2026 katika Kampasi ya Edwad Moringe chuoni hapo Mkoani Morogoro, amesema kuwa wanawake ni kundi muhimu katika jamii na taifa kwa ujumla na nguzo muhimu katika kufanikisha majukumu kiutawala.

Prof. Mabiki ameishukuru Menejimenti ya SUA kwa kutoa fursa ya wanawake wa chuo hicho kupima afya zao bila malipo kwa kuwa fursa hiyo itawasaidia wanawake kuwa sawa kiafya na kumfanya mwanamke kufanya kazi vizuri na kwa ufanisi ili kuhakikisha Dira ya mwaka 2050 inafikia malengo.

Aidha kwa upande wake Dkt. Elimwidimi  Swai ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake kutoka hospital ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo amefundisha athari za magonjwa mbalimbali ya uzazi ikiwemo Kansa ya shingo ya kizazi itokanayo na maambukizi ya virusi vya (HPV) ambapo amewataka wanawake kupima afya zao mara kwa mara kwani magonjwa hayo yanagundulika mapema  na yanatibika kwa haraka.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto SUA  Dkt. Graca Chotamawe amesema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), asilimia 70 ya watu millioni 41 wanakufa kwa mwaka kwa magonjwa yasiyo ambukiza kutokana na kukua kwa teknolojia ya vyakula na ulaji, na namna ya kuishi wakiwa katika shughuli za kila siku.

 Aidha ametoa wito kwa wanawake kutambua namna bora ya kuepuka magonjwa hayo ikiwemo kula vyakula asilia na kufanya mazoezi ya mwili ili kupunguza vifo na umaskini nchini na kuwataka elimu hiyo ikawasaidie kiafya na jamii zinazowazunguka.

Kwa upande wake Bw. Faraja Kamendu ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi (RAAWU) tawi la SUA amesema kuwa kongamano hilo ni chachu ya kuimarisha mtandao wa wanawake wanaojitambua kwani wana uwezo wa kutimiza majukumu kwa ufanisi na kwa ubora na kuahidi ushirikiano katika kila hatua ya maendeleo.

Hatua hiyo pia inaonesha dhamira ya chuo katika kuunga mkono ustawi wa wanawake huku kikielekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayofanyika tarehe 8 Machi 2026 ambayo kwa mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo “Haki kwa Wanawake na Wasichana Msingi wa Maendeleo Jumuishi kufikia Dira 2050”.


MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA KONGAMANO HILO.

Dkt. Elimwidimi  Swai ambaye ni Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi na wanawake kutoka hospital ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo akifafanua jambo kwenye kongamano hilo wakati akiwasilisha mada yake.

Daktari bingwa wa magonjwa ya watoto SUA  Dkt. Graca Chotamawe akiwasilisha mada yake kwenye kongamano hilo.









Post a Comment

0 Comments