Na: Ngolo Mboje
Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kimezindua
mradi wa kubadilisha taka hai kuwa chakula cha mifugo na mbolea hai kwa kutumia
teknolojia ya BSF, ikiwa ni
jitihada za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kupunguza uzalishaji
wa gesi joto na kuboresha usimamizi wa taka.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Januari 28, 2026 mjini Morogoro Dkt. Hamis Tindwa, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Masomo ya Shahada za Awali, ameipongeza Menejimenti ya SUA kwa kuanzisha mradi huo muhimu unaolenga kuwanufaisha wakulima na wafugaji akiahidi ushirikiano wa karibu, na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Prof. Robert Max, Mkurugenzi wa Mradi kutoka Ndaki ya Mifugo na Afya ya Wanyama SUA, amesema lengo kuu la mradi huo ni kuchakata taka hai na kuzalisha chakula bora cha mifugo pamoja na mbolea hai kwa ajili ya kilimo.
Ameeleza kuwa wananchi watanufaika pia kupitia elimu itakayotolewa juu ya namna ya kuzalisha na kukusanya taka hizo kwa matumizi ya mradi.
Aidha, Prof. Max ameishukuru Menejimenti ya SUA kwa kutoa ushirikiano katika ujenzi wa eneo maalum la kuchakata taka hizo kwa kushirikiana na Manispaa ya Morogoro, akisema kuwa ushirikiano huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza changamoto ya uzalishaji wa taka nyingi katika mkoa wa Morogoro.
Naye Bi.
Elizabeth Elias Ngobi, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro, ameishukuru
SUA kwa kuanzisha na kuzindua mradi huo, akieleza kuwa utawanufaisha wananchi
wa mkoa huo hususan wakulima na wafugaji kwa kupata chakula cha mifugo na
mbolea bora kwa bei nafuu.
Ameongeza kuwa manispaa iko tayari kushirikiana na waratibu wa mradi kuhakikisha unafanikiwa na kuleta manufaa endelevu kwa manispaa na mkoa kwa ujumla.
Kwa ujumla, uzinduzi wa mradi huu unatarajiwa
kuleta tija kubwa mkoani Morogoro kwa kuimarisha kilimo na ufugaji, kutengeneza
fursa za kiuchumi kwa wananchi, na kupunguza changamoto ya taka, sambamba na
kuchangia juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
.webp)

%20(1).webp)
.webp)
.webp)
.webp)
0 Comments