Na: Ayoub Mwigune
Ushirika wa Wahitimu Wajasiriamali wa Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUGECO) unaendelea kuimarisha ushirikiano wake na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kwa lengo la kuwawezesha vijana, hususan wanafunzi wa uhandisi wa kilimo,
kujiajiri kupitia kilimo cha umwagiliaji kinachotumia mifumo ya kisasa.
Ushirikiano huo unalenga kuwajengea vijana ujuzi wa vitendo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuchangia upatikanaji wa ajira endelevu katika sekta ya kilimo, hasa katika maeneo yanayokabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa mvua za uhakika.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kijana Mkulima, Mkurugenzi Mtendaji wa SUGECO, Revacatus
Kimario, amesema ushirikiano kati ya SUGECO na SUA umechangia kwa kiasi kikubwa
kuwajengea vijana utaalamu unaohitajika katika utekelezaji wa miradi ya kilimo
cha umwagiliaji.
Ameeleza kuwa wataalamu wengi wanaotekeleza miradi hiyo ni wahitimu wa SUA, jambo linalothibitisha mchango wa chuo katika kuandaa rasilimali watu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya sekta ya kilimo.
Kimario amesema SUGECO imeandaa maadhimisho ya Siku ya Kijana Mkulima (Youth Farmers Field
Day) kupitia Mradi wa Kizimba
Business Model (KBM) unaofadhiliwa na Beyond Farming Collective (BFC). Hafla hiyo imefanyika Januari 23,
2026 katika shamba la mradi wa vijana lililopo kijiji cha Lubungo, wilayani
Mvomero, mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa Kimario, lengo la tukio hilo ni kuonesha maendeleo, changamoto na mafanikio ya utekelezaji wa Mfumo wa Biashara wa Kizimba (KBM), pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya vijana, wadau wa maendeleo na taasisi zinazohusika na sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Siritamu Yohane, Afisa Kilimo, Huduma za
Ugani Wilaya ya Mvomero, akizungumza kwa niaba ya Afisa Kilimo, Mifugo na Uvuvi
wa wilaya hiyo, amesema mradi huo hauwanufaishi vijana pekee bali unagusa jamii
nzima kwa ujumla. Amefafanua kuwa vijana wengi wanatoka katika familia, hivyo
kijana anaponufaika kiuchumi kupitia mradi huo, familia na jamii nzima
hunufaika pia.
Mkazi wa kijiji cha Lubungo, Jenirosa Abiasi, amesema utekelezaji wa mradi huo katika eneo lao unatarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika kilimo, hasa ikizingatiwa kuwa kijiji hicho hakipati mvua za uhakika mara kwa mara.
Ameeleza kuwa kupitia kilimo cha umwagiliaji, wakazi wanatarajia kuongeza uzalishaji na kupata matokeo chanya ikilinganishwa na kilimo cha awali cha mbaazi na mahindi ambacho hakikuwa na mafanikio makubwa.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Lubungo, Kanuti Barnabas,
amesema kijiji kimeupokea kwa mikono miwili mradi wa SUGECO, akibainisha kuwa
mradi huo unawasaidia wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na kuelekea kwenye
kilimo cha kisasa chenye tija.
Ameongeza kuwa serikali ya kijiji iko tayari kushirikiana na
SUGECO katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo itakayowanufaisha
vijana, wanawake na wakazi wa kijiji hicho kwa ujumla.









0 Comments