Na: Adam Maruma
Katika
kuadhimisha miaka 200 ya zao la karafuu duniani, Chuo Kikuu cha Sokoine cha
Kilimo (SUA) kimekutana na wadau mbalimbali wanaojihusisha na uendelezaji wa
zao hilo ili kujadili njia bora za kuhamasisha jamii kuona na kutumia fursa
zinazopatikana katika zao la karafuu, linalotajwa kuwa miongoni mwa mazao ya
kimkakati katika Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mkuu wa Ndaki ya Kilimo SUA, Dkt. Nyambilila Amuri, amesema kikao hicho kimejadili namna ya kulienzi na kulifufua zao la karafuu ili liwe chanzo cha fursa za kiuchumi kwa wakulima na wananchi wengine wa Mkoa wa Morogoro.
Dkt. Nyambilila amesema
Ndaki ya Kilimo imeona fursa kubwa katika zao hilo kwa kuwa ni miongoni mwa
mazao ya viungo (spice crops) yanayofundishwa katika Ndaki hiyo,
na pia ni zao lenye thamani kubwa kiuchumi. Ameeleza kuwa kukutana na wadau hao
kumewapa faraja na kuahidi kuendeleza ushirikiano na taasisi mbalimbali
zinazohusika na uendelezaji wa zao la karafuu.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Shirika la Umoja Conservation Trust, Bryan Bwana, amesema wamefika SUA kuanzisha mpango wa pamoja ikiwa ni pamoja na kubuni sera kabambe ya uendelezaji wa zao la karafuu. Amesema zao hilo lina faida nyingi kwa wananchi, na anaamini mpango huo utafanikiwa kwa kuwa SUA ni Chuo kikongwe chenye wataalamu wabobezi katika nyanja mbalimbali za kilimo.
Ameongeza kuwa zao la karafuu, linalotimiza miaka 200 ya kuwepo kwake mwaka huu, lina faida lukuki, na endapo wananchi wataelimishwa na kung’amua fursa zilizopo, linaweza kuwa mdau muhimu wa maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Naye Mshauri wa Kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Peter Gama, amesema mkoa umeendelea kuchukua jitihada mbalimbali za kuendeleza zao la karafuu kutokana na umuhimu wake wa kimkakati.
Miongoni
mwa jitihada hizo ni kugawa miche ya karafuu bure kwa wakulima pamoja na kwa
baadhi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza kupitia mradi wa “Jisomeshe na
Mkarafuu”, ulioanzishwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Umoja Conservation Trust, Tanzania Environmental Expert Association pamoja na wanataaluma wa SUA. Katika kikao hicho, pia ilijadiliwa mikakati ya kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu fursa za zao la karafuu kupitia shughuli kama kuanzishwa kwa mashindano ya michezo ya Karafuu Cup, Karafuu Marathon pamoja na kuendeleza utalii wa karafuu.
Zao la karafuu linajulikana kulimwa zaidi Zanzibar, huku Mkoa wa Morogoro ukiwa miongoni mwa maeneo ya Tanzania Bara yanayolima zao hilo.
0 Comments