Na: Asifiwe Mbembela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, ametoa rai kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya Sayansi ya Wanyama, Viumbe Maji na Nyanda za Malisho kwamba hawatapoteza muda kwa kusoma katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kwani sekta hizo zina wigo mpana wa fursa za ajira na uwekezaji.
Balozi Dkt. Bashiru ameyasema hayo alipokutana na wanafunzi wa mwaka wa pili wa Shahada ya Usimamizi wa Nyanda za Malisho waliokuwa kwenye mafunzo ya vitendo ya upandaji wa mbegu za malisho aina ya alfalfa, zenye uwezo wa kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa mifugo, wakati wa ziara yake ya siku moja chuoni hapo.
Katika mazungumzo hayo, aliwahimiza wanafunzi hao kuwekeza ipasavyo katika
maarifa wanayoyapata kwa kuyafuatilia kwa umakini, ili waweze kung’amua na
kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nyanda za malisho, ambayo inaendelea
kukua kutokana na ongezeko la mahitaji pamoja na athari za mabadiliko ya
tabianchi.
"Mnayoyasoma hapa msidhani mnapoteza muda, hili eneo la malisho sasa litakuwa ni biashara kubwa na waliochangamkia wamenza kupata biashara hiyo. Kuna biashara ya mbegu zake, biashara ya malisho yenyewe na nyinyi hapa mnafundishwa namna ya kuyasindika ili kuyaongezea thamani, nawapongezeni sana kwa kuchagua kusoma katika eneo hili muhimu kwenye mifugo", amesema Dkt. Bashiru.
Aidha, Balozi Dkt. Bashiru amesema Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimekuwa
kikiiunga mkono Serikali katika utekelezaji wa sera na mikakati ya maendeleo,
ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 inayosisitiza mabadiliko ya mifumo
ya ufugaji kutoka mfumo wa kiasili kwenda ufugaji wa wanyama wachache wenye
tija kubwa.
Akizungumza katika ziara hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Raphael Chibunda, amesema kuwa licha ya Chuo kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa bajeti unaotokana na utekelezaji wa majukumu mbalimbali, SUA imekuwa ikitenga shilingi bilioni 1 kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kuwawezesha watafiti wachanga kuomba na kutumia fedha hizo katika kufanya tafiti zao.




0 Comments