Na: Farida Mkongwe
Watafiti
kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Wizara ya Maji, pamoja na wadau
mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa taasisi za kimataifa wamekutana jijini
Dodoma kupokea matokeo ya awali ya tafiti na kujadili mbinu shirikishi za
kutatua changamoto za upatikanaji wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi
kupitia Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya
Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY).
Akifungua mkutano huo Oktoba 7, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Rosemary Rwebugisa, amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka na za pamoja kukabiliana na changamoto ya maji nchini, hususan katika maeneo kame kama Dodoma, “Tanzania ina takribani mita za ujazo bilioni 126 za maji kwa mwaka, lakini mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi zisizo endelevu vinatishia upatikanaji wa rasilimali hii muhimu, mfano mahitaji ya maji jijini Dodoma yamefikia lita milioni 149.5 kwa siku huku uzalishaji ukiwa ni milioni 79.1 pekee”.
Akitoa salamu kutoka SUA, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha na Utawala) Prof. Amandus Muhairwa, amesema SUA itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kufanya tafiti zenye tija kwa jamii na kuleta suluhisho bunifu kwa changamoto za mabadiliko ya tabianchi na upungufu wa maji, “ tafiti hizo hufanywa kwa ushirikiano na taasisi za ndani na nje ya nchi, zikiwa na lengo la kuboresha maisha ya Watanzania kupitia sayansi na teknolojia”.
Kiongozi Mkuu wa Mradi wa CLARITY, Prof. Japhet Kashaigili, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu SUA, amesema matokeo ya awali ya tafiti yatawezesha wadau kutafakari hatua zilizofikiwa, kuainisha changamoto, na kubuni mikakati ya pamoja inayolenga kufanikisha malengo ya mradi huo.
“Mkutano huu ambao pia
umemuhusisha mwakilishi wa mfadhili wa mradi huu, Dkt. Mercy Ojoyi, ni sehemu muhimu
ya mfululizo wa majadiliano ya kitaalamu yanayochochea mageuzi ya kifikra na
kisera kuhusu mabadiliko ya tabianchi, usimamizi wa maji na maendeleo endelevu,”
amesema Prof. Kashaigili.
Kwa upande wake, Mtafiti Msaidizi wa Mtafiti Kiongozi wa Mradi wa CLARITY kutoka SUA, Dkt. Devota Mosha, akiwasilisha malengo ya mradi, amesema CLARITY unalenga kujumuisha matokeo ya tafiti katika sera na mipango ya maendeleo ya maji ili kuchochea mfumo wa usawa, stahimilivu na endelevu wa utunzaji wa maji chini ya ardhi, “ ushirikiano wa karibu kati ya watafiti, Serikali na wadau wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha matokeo ya utafiti yanachangia moja kwa moja katika kuboresha maisha ya wananchi”.
Matokeo ya awali yaliyowasilishwa katika mkutano huo yanahusu mifumo ya kijamii na kihaidrojia ya rasilimali za maji chini ya ardhi ikiwemo upatikanaji, athari za mabadiliko ya tabianchi na mbinu bora za usimamizi wake, njia za maendeleo ya maji kwa ajili ya kuboresha upatikanaji, pamoja na modeli za kuchakata maji chini ya ardhi zinazotumika kutathmini upatikanaji na ustahimilivu wa maji katika jiji la Dodoma.
Picha zote na Tatyana Celestine Manda
0 Comments