SUAMEDIA

SUA yaendelea kuonesha fursa mpya zilizopo kwa vijana

 Na: Josephine Mallango

Vijana zaidi ya 1,000 nchini watanufaika na mabadiliko ya kiuchumi kupitia mradi mpya wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH, unaotekelezwa chini ya RUFORUM kwa ufadhili wa Mastercard Foundation, wakiwemo vijana kutoka vikundi 18 katika Halmashauri ya Mji Ifakara, mkoani Morogoro.

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ambao ndiyo wenyeji wa mradi huo, wakati wa utambulisho Ifakara wamepongezwa na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dunstan Kyobya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina ya mafunzo kwa vijana wa Ifakara, ambapo amewataka vijana waliochaguliwa kushiriki katika mafunzo hayo kutumia maarifa watakayopata kuongeza ubunifu katika kutafuta masoko ya bidhaa zao, kupata mitaji na matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wao.

“Wataalamu wetu kutoka SUA mkiongozwa na maprofesa na madaktari mlioko hapa, fikisheni salamu za pekee kwa Prof. Chibunda na uongozi wote wa SUA kwa namna mmeona vijana wa Ifakara wanafaa kuwemo katika kunufaika na mabadiliko ya kiuchumi kwa kuleta fursa mpya ya kuongeza mnyororo wa thamani na upatikanaji wa masoko katika mpunga na mboga mboga. Vijana wangu wa Ifakara mpo? Msihishie kunywa chai na kupiga picha kwenye semina hii; tunataka mabadiliko! Mafunzo haya yakawape pesa mtakapoongeza uzalishaji wenu,” amesema Wakili Kyobya.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi kutoka SUA, Dkt. Hamisi Tindwa, amesema mradi huo unalenga kuwajengea vijana uwezo wa kuendesha biashara endelevu na ubunifu katika kutafuta masoko kwenye sekta ya kilimo, badala ya kubaki katika uzalishaji pekee huku wakilalamika kukosekana kwa soko na ubunifu katika bidhaa zao.

“Mradi huu umelenga vijana katika vikundi, na falsafa ya mradi ni kushughulika na vijana kuanzia miaka 18–35, huku asilimia 70 wakilengwa vikundi vya vijana wa kike.

Katika kipindi cha miaka mitano, pia tutaenda kwa hatua na uwezekano wa kujenga mitaji, matamanio yetu baada ya mradi kuisha ni kuona mafanikio kwa vikundi hivi kuwa kampuni za uzalishaji na kufanya shughuli zao kupitia kampuni zao wenyewe, ambapo mradi huu utawanufaisha vijana kutoka wilaya tatu za Morogoro na Mpimbwe wilayani Mlele mkoani Katavi,” amesema Dkt. Tindwa.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Florence Mwambene, amesema watasimamia vikundi hivi ili kufikia malengo ya mradi unaotoa fursa kwa vijana, kwa kuwa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wameona uelewa walionao na utaalamu wao waushushe kwenye ngazi ya jamii, hasa kwa vikundi, watoe elimu ya kuongeza uzalishaji, ubunifu pamoja na masoko ya uhakika ili kuongeza wigo wa fursa kwa vijana kujiajiri na kuajiri wengine.

Amesema kuwa Ifakara mradi una vikundi kutoka kata nne za Kiberege, Katindiuka, Kisawasawa na Signal.

Kwa upande wa vikundi vya vijana kutoka katika kata hizo nne, wakati wa mafunzo wameainisha baadhi ya changamoto zinazowakabili kwa sasa ambazo ni kulima kwa mazoea bila kutumia mbegu bora jambo linalowapelekea kupata mavuno machache, kukutana na magonjwa ikiwemo mnyauko na fangasi, matumizi ya viuatilifu na mbolea zisizo sahihi pamoja na kukosa masoko.

Wamesema wana imani na SUA kupitia mradi huo watapata utatuzi wa changamoto hizo ili wazalishe mazao ya kutosha na ziada.

Mradi wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH ni sehemu ya programu ya RUFORUM inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo cha Nelson Mandela (Arusha), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na Jukwaa la Vyuo Vikuu Afrika (RUFORUM) kwa ufadhili wa Mastercard Foundation una thamani ya shilingi bilioni 1.6, na unatekelezwa katika halmashauri nne nchini ambazo ni Halmashauri ya Morogoro Vijijini, Halmashauri ya Mji Ifakara, Manispaa ya Morogoro, na Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele, mkoani Katavi.






Picha zote na Ayoub Mwigune

Post a Comment

0 Comments