SUAMEDIA

DC Morogoro: Elimu msingi wa kudhibiti mabadiliko ya tabianchi

 Na: Farida Mkongwe

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, amesema mabadiliko ya tabianchi yameendelea kuathiri kwa kiwango kikubwa ustawi wa jamii na mazingira, hivyo kuwataka wananchi kuacha tabia ya uchomaji moto kwenye milima, uharibifu wa vyanzo vya maji na kutofanya shughuli za kibinadamu katika maeneo yasiyostahili ili kulinda mustakabali wa mazingira.


Akizungumza baada ya kufunga Kongamano la Pili la Kisayansi la Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano lililofanyika mjini Morogoro, Kilakala pia amekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuwa mwenyeji wa kongamano hilo muhimu na kusema SUA imeonesha uongozi na dhamira kubwa katika kushirikiana na vyuo vikuu vingine na wadau wa kimataifa kujadili masuala ya tabianchi na maendeleo endelevu.

“Msingi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni elimu, hivyo jamii nzima inapaswa kushirikiana katika kuelimisha wananchi ili wajue athari za vitendo vyao kwa mazingira kwani jukumu la kulinda mazingira si la Serikali pekee, bali ni la kila mmoja”, amesema Kilakala.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano hilo, Prof. Japhet Kashaigili kutoka SUA, amesema kongamano hilo limeweka maazimio muhimu yatakayotekelezwa kwa vitendo.

Miongoni mwa maazimio hayo ni kuendeleza programu za ubadilishanaji wa wanafunzi na walimu ili kujenga uwezo wa pamoja, kuanzisha vituo vya teknolojia na ubunifu, pamoja na kuandika maandiko ya pamoja ya utafiti yanayolenga kutoa suluhisho la changamoto za jamii.

Ameyataja maazimio mengine kuwa kongamano litachambua masuala ya kisera yanayohitaji kuwasilishwa serikalini, hususan katika maeneo ya afya, maji na mabadiliko ya tabianchi, ili kusaidia Serikali kuunda sera shirikishi zinazotokana na tafiti za kitaalamu.



Naye Dkt. Safiness Simon Msollo, Mhadhiri Mwanadamizi kutoka SUA ambaye ameshiriki kongamano hilo amesema mafunzo ya kongamano hilo yametoa mwanga mkubwa juu ya umuhimu wa kuunganisha matokeo ya tafiti na jamii akisisitiza kuwa tafiti hazipaswi kubaki kwenye maktaba pekee, bali lazima ziwe endelevu na ziwe na mchango wa moja kwa moja kwa wananchi.

Kongamano lijalo ambalo litakuwa la Tatu la Kisayansi la Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano litafanyika katika Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika (NM-AIST) jijini Arusha.







Post a Comment

0 Comments