Na:
Ayoub Mwigune
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo
(SUA) kimepokea wataalam wawili wa lugha kutoka nchini Cuba, watakaofundisha
lugha ya Kihispania kwa kipindi cha miaka miwili chini ya Idara ya Lugha,
katika jitihada za kuendeleza elimu ya kimataifa na kuboresha umahiri wa lugha
miongoni mwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa hafla ya
kuwapokea, Mratibu wa Kitengo cha Umaitaifishaji na Majalisi wa SUA, Prof.
Jonathan Mbwambo, amesema ujio wa wataalam hao ni sehemu ya mwendelezo wa
ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Cuba, unaolenga kuimarisha elimu,
utafiti na urafiki wa kimataifa.
Amesema SUA inatambua umuhimu wa
lugha ya Kihispania katika mawasiliano ya kimataifa na inahamasisha wanafunzi
kutumia fursa hiyo kujifunza lugha hiyo, ambayo ni miongoni mwa lugha
zinazozungumzwa zaidi duniani.
Kwa upande wao, wataalam hao, Bi.
Yusimà Vigoa Maruri na Bw. Lázaro Nochea Vilella, wameeleza namna walivyo
furahishwa na mapokezi mazuri waliyoyapata SUA pamoja na fursa ya kushirikiana
na walimu na wanafunzi katika kukuza elimu ya lugha na tamaduni.
Bi. Maruri amesema wamejipanga
kuhakikisha wanafunzi wa SUA wanapata ujuzi wa kina wa lugha ya Kihispania na
uelewa wa tamaduni za Cuba na Amerika ya Kusini, wakiamini kuwa ni msingi
muhimu katika mawasiliano ya kimataifa na fursa za ajira duniani.
0 Comments