Na: Farida Mkongwe
Kampuni ya Afya ya
Mnyama Digital Limited, imekipongeza
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa mchango wake mkubwa katika kuwajengea vijana ujuzi na uwezo wa ubunifu
unaochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Akizungumza katika mkutano wa mwaka wa SUA CEO Alumni Forum 2025, Mwanzilishi Mwenza na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Juliet Tarimo, amesema elimu aliyoipata SUA imekuwa chachu muhimu katika mafanikio yake binafsi na ya kampuni yake.
Amesema amefurahia kuona jinsi SUA ilivyowakutanisha
wahitimu wa miaka mbalimbali, wakiwemo wakurugenzi na watendaji wanaoendelea
kuchangia maendeleo ya taifa kupitia sekta tofauti.
“SUA imenijenga kielimu na kimfumo, kupitia somo la Agriculture
Investment and Banking, niliweza kupata maarifa yaliyoniwezesha kuunda
kampuni inayotumia teknolojia kusaidia wafugaji,” amesema Juliet.
Kampuni ya Afya ya Mnyama Digital Limited inalenga kuboresha ustawi wa wafugaji kwa kutumia teknolojia ya kidigitali kufuatilia maendeleo ya afya ya mifugo.
Kupitia mfumo huo, wafugaji wanapata taarifa sahihi kuhusu
afya za mifugo yao, hatua za matibabu, chanjo na ushauri wa kitaalamu ambao
unalenga kuongeza tija katika uzalishaji na kupunguza hasara zinazotokana na
magonjwa yasiyotambuliwa mapema, hivyo kuendeleza lengo la taifa la kuongeza
uzalishaji wa mifugo wenye ubora na faida.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji huyo amewasisitiza wanafunzi wa
SUA kutumia ipasavyo rasilimali zilizopo
chuoni, ikiwemo walimu, maabara, na program za mafunzo kwa vitendo, ili kukuza
ubunifu unaoweza kuleta mabadiliko makubwa katika jamii.
0 Comments