Na: Farida Mkongwe
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimeendelea kuthibitisha nafasi yake kama chimbuko la viongozi, wabunifu na wataalamu wanaoleta mabadiliko nchini kupitia mkutano wa mwaka wa SUA CEO Alumni Forum 2025 uliofanyika chuoni hapo.
Akifungua
mkutano huo Oktoba 13, 2025, uliohusisha wanafunzi waliowahi kusoma SUA ambao
sasa ni wakuu wa taasisi mbalimbali (CEO Alumni), Rais wa Majalisi ya SUA, Prof. Madundo Mtambo, amewapongeza
wahitimu waliopanda vyeo au kushika nafasi za juu za uongozi katika sekta za
umma na binafsi, akisema mafanikio yao ni kielelezo cha ubora wa elimu na
maadili ya SUA.
Katika
hotuba yake, Prof. Mtambo ametumia fursa hiyo kuwakumbuka wahitimu
waliotangulia mbele ya haki tangu mkutano uliopita, akisema mchango wao
utaendelea kuthaminiwa na kuwa dira kwa vizazi vijavyo, pamoja na kuwahimiza
wahitimu wote kudumisha mshikamano na kuendelea kuchangia maendeleo ya SUA kwa
kutumia ujuzi, ubunifu na uzoefu walioupata chuoni hapo.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalam SUA, Prof. Maulid Mwatawala, ameeleza kuwa Chuo hicho kimeanzisha mageuzi makubwa ya mitaala ili kuongeza ujuzi wa vitendo kwa wanafunzi.
Amesema
mafunzo kwa vitendo sasa yamepanuliwa kutoka wiki tano hadi muhula mzima wa
masomo, na wataalamu kutoka sekta ya viwanda na biashara wameanza kushirikishwa
moja kwa moja katika kufundisha, “lengo ni kuhakikisha wahitimu wa SUA wanakuwa
tayari kwa soko la ajira na wana uwezo wa kutatua changamoto halisi za jamii”.
Prof. Mwatawala amesisitiza kuwa mageuzi ya mitaala yamelenga kuondoa mfumo wa kukariri na kuandika mitihani, na badala yake kuweka mkazo kwenye tathmini endelevu, kazi za vitendo na tafiti za ubunifu, “kwa wanafunzi wa Shahada za Juu, mfumo mpya unawahamasisha kujikita zaidi katika tafiti na semina zitakazowaongezea uwezo wa kuchambua na kutatua changamoto za kijamii kwa kutumia sayansi na teknolojia,” amesema.
Akitoa
shukurani kwa niaba ya SUA CEO Alumni Forum 2025, Prof. Fatihiya Massawe, Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na
Utawala katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama, ameelezea furaha yao ya kufika SUA
na kuona chuo kikiendelea kung’ara, “kila mwaka Chuo kimekuwa kikiimarika zaidi
katika ubunifu na utoaji wa elimu bora, sisi wahitimu tupo tayari kushirikiana
na kusaidia chuo katika kuendeleza ubora wa elimu, utafiti na huduma kwa
jamii,” amesema.
Wakuu hao wa taasisi mbalimbali pia wamepata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo ya SUA, ikiwemo Idara ya Shamba la Mafunzo ambako walijionea shughuli mbalimbali za ufugaji na kilimo, kutembelea shamba la malisho na uzalishaji wa mifugo, maabara ya kuzalisha vifaranga vya samaki, mabwawa ya ufugaji wa samaki pamoja na studio ya mafunzo kwa vitendo ya Nguo na Ngozi (Textile and Leather Studio) ambako walijionea ubunifu wa wanafunzi na walimu katika kuzalisha bidhaa za thamani kwa kutumia malighafi za ndani.




.jpg)




0 Comments