SUAMEDIA

Vijana watakiwa kutumia elimu ya SUA kujikomboa kiuchumi

 Na: Josephine Mallango

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ifakara Mjini, Said Majaliwa, amewahimiza vijana nchini kutumia maarifa na fursa za elimu zinazotolewa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ili kuongeza tija katika uzalishaji wa kilimo na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya Mradi wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH kwa vikundi vinne vya vijana kutoka Ifakara, Majaliwa alisema SUA ni kitovu cha elimu nchini, hivyo vijana wanapaswa kutumia wingi wa maarifa yaliyopo chuoni hapo katika kuongeza ufanisi na ubunifu katika shughuli za kilimo.

“Vijana wa Ifakara sasa ni wakati wenu wa kuinuka kiuchumi. Zingatieni elimu iliyotolewa na SUA; chuo cha SUA kina elimu kubwa na nyingi. Ukiweza kuchukua elimu yao kwa uchache pale unapohitaji na kuitumia, unafanikiwa. Kwa wingi wa elimu waliyonayo huwezi kumaliza yote, ila chukua ya mahitaji yako uitumie ufanikiwe,” amesema Majaliwa.

Naye Mwenyekiti wa Kikundi cha Umoja wa Mafundi Ujenzi Kiberege Bwawani, ambacho kinajihusisha na kilimo cha mpunga, amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupata mavuno hafifu licha ya kutumia nguvu nyingi ambapo ametoa ombi kwa SUA kusaidia katika kutatua changamoto za mitaji midogo, matumizi ya viwatilifu visivyofanya kazi ipasavyo, na upatikanaji wa soko la uhakika kwa mazao yao.

Kwa upande wake, Kiongozi Mshiriki wa Mradi huo, Dkt. Nyambilila Amuri, amesema mradi huo wa miaka mitano unalenga kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika kupanua mnyororo wa thamani wa kilimo, kupitia mazingira rafiki, teknolojia bunifu, na stadi muhimu zitakazowawezesha kufanya kilimo kwa tija na kuchangia maendeleo ya taifa.

Dkt. Nyambilila ameeleza kuwa changamoto ya masoko inaweza kutatuliwa kwa ubunifu na kuboresha ubora wa mazao ili kuvutia wateja na kupata masoko ya kudumu.

“Masoko nchini bado yapo mengi kutokana na kuongezeka kwa uhitaji wa mazao ya kilimo. Kwa mfano, kijana anaweza kutafuta tenda ya kusambaza mboga mboga katika shule za msingi zinazotoa huduma ya chakula. Ukiboresha mazao yako, uuzaji utakuwa rahisi,” amesema Dkt. Nyambilila.

Aidha, ameongeza kuwa changamoto ya baadhi ya viwatilifu kushindwa kutibu magonjwa itatatuliwa kupitia tafiti endelevu, kwa kuwa katika kilimo hawatumii sumu za kudumu ili kulinda afya za walaji, hivyo tafiti hizo zinahitaji muda ili kutoa suluhisho la kudumu.

Mradi wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH ni sehemu ya Programu ya RUFORUM, inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya SUA, Chuo cha Nelson Mandela (Arusha), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na Jukwaa la Vyuo Vikuu Afrika (RUFORUM), kwa ufadhili wa Mastercard Foundation wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.6.

Mradi huu unatekelezwa katika halmashauri nne nchini ambazo ni Halmashauri ya Morogoro Vijijini, Halmashauri ya Mji Ifakara, Manispaa ya Morogoro, na Halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele, mkoani Katavi.

 


 

Post a Comment

0 Comments