Na: Ayoub Mwigune
Chuo
Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimezindua rasmi Mradi wa Mtandao wa Wadau wa Utafiti wa Kilimo Ikolojia katika Afrika
Mashariki (Regional Multi-Actor Research Network on Agroecology in East Africa
– RMRN-EA) kupitia warsha ya siku moja iliyofanyika chuoni hapo,
ikihusisha watafiti, watunga sera, wakulima na wadau mbalimbali wa sekta ya
kilimo.
Warsha hiyo imelenga kuimarisha utafiti wa kilimo ikolojia (agroecology) na kuongeza ushirikiano kati ya taasisi za elimu, utafiti, wakulima na jamii, ili kukuza tija ya kilimo na kupunguza athari za kimazingira.
Akizungumza
wakati wa uzinduzi huo, Prof. Japhet
Kashaigili, Kiongozi wa Mradi wa RMRN-EA, amesema mradi unalenga
kuendeleza mitaala ya agroecology,
kujenga mtandao wa utafiti na kubadilishana maarifa kati ya nchi washiriki.
Amesema mradi utasaidia kukuza ushirikiano wa watafiti, watunga sera, wakulima na jamii, huku ukihakikisha ushiriki wa wanawake angalau asilimia 30 katika shughuli zote na kwamba utachangia maboresho ya sera na uvumbuzi katika kilimo ikolojia kote Afrika Mashariki.
Kwa
upande wake, Prof. Maulid Mwatawala,
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu) SUA, amepongeza
mradi huo kwa kujikita katika vipengele vinavyohakikisha ufanisi na uendelevu.
Amesema mradi unazingatia usawa wa kijinsia, ushirikishwaji wa wadau, na unajikita katika muktadha wa kikanda na kitaifa kupitia ushirikiano wa vyuo vikuu washiriki na pia unalingana na Ajenda Kuu za Maendeleo za Kimataifa ikiwemo SDGs, AU Agenda 2063 na CAADP.
Prof.
Mwatawala amesisitiza kuwa SUA itatoa ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha
mafanikio ya mradi na kuweka mazingira bora ya ushirikiano wa wadau wote.
Mradi
wa RMRN-EA unatekelezwa kwa
ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya Afrika Mashariki ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA)
kwa upande wa Tanzania, Chuo Kikuu cha
Makerere nchini Uganda, na Chuo
Kikuu cha Nairobi nchini Kenya.







0 Comments