SUAMEDIA

Vijana wa Mpimbwe wahimizwa kutumia Mradi wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH kuongeza tija ya kilimo

Na: Josephine Mallango

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, Bi. Shamim Mwariko, amewataka vijana wa Mpimbwe kutumia Mradi wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH unaotekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuongeza uzalishaji ili kupata fursa za masoko ndani na nje ya Tanzania.


“Mradi huu wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH ni mradi wa kipaumbele kwa Mpimbwe, watendaji wote wa Mpimbwe wahakikishe vijana wanawezeshwa ili kupata matokeo mazuri ya mradi huu ambayo ni fursa ya kuonekana na kupata miradi mingine zaidi, wananchi waendelee kunufaika, tuna skimu nne za umwagiliaji, hii ni nafasi yetu tushirikiane na wataalam wa SUA sasa tulete mabadiliko ya kiuchumi Mpimbwe,” amesema Mwariko.

Akizungumza wakati wa kutambulishwa kwa mradi huo mpya unaotekelezwa chini ya RUFORUM kwa ufadhili wa Mastercard Foundation, Mkurugenzi huyo amesema nchi nzima ina halmashauri 184 lakini halmashauri nne pekee ndizo zilizochaguliwa kushiriki katika mradi huo, moja wapo ikiwa Mpimbwe.

Amesisitiza kuwa vijana wa Mpimbwe wanapaswa kutumia mradi huu kama chachu ya kufanikisha ndoto zao kwa kuwa unatoa fursa ya kujiajiri na kuajiri wengine kupitia mnyororo wa thamani wa mazao ya mpunga na bustani, sambamba na matumizi ya teknolojia bunifu za kilimo na usindikaji.

“Vijana ndiyo waendeshaji wa mageuzi ya kiuchumi duniani kote,moja ya vitu ambavyo Afrika inaweza kuuza ndani na nje ya nchi ni mazao ya kilimo, na vijana wa Mpimbwe hawasukumwi kufanya kazi , wanaijua thamani ya pesa ya kilimo, hivyo, mradi huu utapata matokeo mazuri kwa kuwa umejikita kuwawezesha vijana katika kilimo cha tija na mnyororo wa thamani, ambapo hawatatakiwa kutumia nguvu kubwa tena kulima kiholela, bali watatumia teknolojia, ubunifu na kupata masoko ya uhakika kuanzia maandalizi ya mashamba hadi uvunaji na masokoni,” amesisitiza Mwariko.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa wanatarajia matokeo ya mradi huo yatasaidia kuongeza mapato ya halmashauri na kuinua hali ya kiuchumi ya vijana kupitia vikundi vyao, amesema vijana zaidi ya 200 kutoka kata saba za Kibaoni, Ikuba, Chamalendi, Mbede, Mwamapuli, Mamba na Kasansa watanufaika kupitia mafunzo na uwezeshaji wa mradi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe mkoani Katavi.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi, Dkt. Hamisi Tindwa, amesema lengo la mradi ni kuwawezesha vijana kupata ujuzi kupitia mafunzo ya vitendo, kuwapatia mitaji ya kuanzia (mbegu), kuunda ajira za kujiajiri na kuajiri wengine, kuongeza uzalishaji na kuwafikisha kwenye masoko ya uhakika.

Ameongeza kuwa vijana 1,000 wenye umri wa miaka 18 hadi 35 pamoja na wakulima zaidi ya 25,000 watanufaika kupitia mafunzo ya mbinu bora za kilimo na njia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Wakati wa mafunzo kwa vikundi, Naomi James kutoka kikundi cha Upendo Wanawake Iziwasungu kata ya Kasansa, aliomba mradi uwasaidie kwa kuwapatia wataalamu wa elimu sahihi ya kilimo cha mpunga, mbegu bora, matumizi ya viuatilifu na mbolea, pamoja na uwezeshaji wa mitaji na mashine za kuvunia na kuchakata mpunga ili waweze kupata masoko kwa wingi na mazao bora zaidi.

Mradi wa TAGDev 2.0 AGRIFOSE–RIH ni sehemu ya Programu ya RUFORUM inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo cha Nelson Mandela (Arusha), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Jukwaa la Vyuo Vikuu Afrika (RUFORUM) kwa ufadhili wa Mastercard Foundation. Ni mradi wa miaka mitano wenye thamani ya Shilingi bilioni 1.6, unaotekelezwa katika halmashauri nne nchini: Morogoro Vijijini, Ifakara Mjini, Manispaa ya Morogoro na Mpimbwe Wilaya ya Mlele, mkoani Katavi.

  

 



Post a Comment

0 Comments