SUAMEDIA

Utafiti SUA wabaini athari za mabadiliko ya tabianchi kwa maji chini ya ardhi Dodoma

 Na: Farida Mkongwe

Utafiti wa awali uliofanywa na Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY) wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) umebainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu na uratibu hafifu wa taasisi vinachangia changamoto kubwa katika upatikanaji wa maji chini ya ardhi katika Mkoa wa Dodoma.

Akiwasilisha Matokeo ya awali ya utafiti kuhusu mifumo ya kijamii na kihaidrolojia ya rasilimali za maji chini ya ardhi kwenye mkutano wa Maabara ya mabadiliko (Transformation-Lab), Mtafiti Msaidizi wa Mradi wa CLARITY kutoka SUA Evarest Abraham amesema maji ya chini ya ardhi ni chanzo muhimu kinachotoa zaidi ya asilimia 97 ya maji safi duniani, ambayo  yanahudumia zaidi ya watu bilioni 2.5 kote ulimwenguni.

Katika bara la Afrika, hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara, takribani asilimia 70 ya watu hutegemea maji haya kwa matumizi ya kila siku huku kwa upande wa Dodoma, utegemezi huo ni mkubwa zaidi kutokana na hali ya ukame na uhaba wa vyanzo vya maji ya uso kama mito na mabwawa.

Utafiti huo uliohusisha kaya 500 kutoka maeneo ya vijijini na mijini, majadiliano ya vikundi na mahojiano, umeonesha kuwa hali ya hewa imebadilika sana katika kipindi cha miaka 30 iliyopita huku takwimu za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zikionesha mabadiliko makubwa katika mvua na joto, hali ambayo imethibitishwa pia na mitazamo ya jamii.

Kwa mujibu wa utafiti huo, upatikanaji wa maji bado ni changamoto ambapo ni kaya moja pekee kati ya tano mjini na moja kati ya sita vijijini zinazopata maji ya bomba majumbani, huku visima binafsi vikionekana ni vingi zaidi katika maeneo ya mijini, jambo linaloashiria tofauti ya kiuchumi kati ya wakazi wa mjini na vijijini.

Kwa upande wa utawala wa maji chini ya ardhi, utafiti umebaini kuwepo kwa udhaifu katika usimamizi na uratibu. Taasisi rasmi kama DUWASA, RUWASA na Serikali za mitaa zinafanya kazi zao kwa utaratibu, lakini mara nyingi zinakosa uratibu wa pamoja na rasilimali za kutosha kufuatilia matumizi ya maji.

Matokeo hayo ya awali yanaonesha pia kuwa asilimia 55 ya watumiaji wa maji ya chini ya ardhi waliripoti kuwa utawala wa maji ni hafifu, huku ushiriki wa wanawake, vijana na makundi maalum ukiwa mdogo, hali inayochangia kudhoofika kwa uendelevu na usawa katika usimamizi wa rasilimali hizo.

Aidha utafiti huo umependekeza Wizara ya Maji kushirikiana na sekta binafsi kupitia mfumo wa ushirikiano kati ya umma na binafsi (PPP) ili kuongeza upatikanaji wa huduma za maji,  Serikali kusaidia kaya zenye kipato cha chini kuunganishwa na huduma za maji ya bomba, kuimarisha utekelezaji wa malengo ya usimamizi wa rasilimali za maji nchini na  kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya wizara, taasisi za Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na jamii kupitia kubadilishana taarifa na kufanya maamuzi kwa pamoja.





Picha zote na Tatyana Celestine Manda

Post a Comment

0 Comments