SUAMEDIA

SUA yalipa fidia ya Bilioni 1.7 Mpimbwe mkoani Katavi

 Na Gerald Lwomile:

Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimelipa fidia ya ardhi  ya shilingi za kitanzania Bilioni 1.7 kwa wananchi wa maeneo ya Kibaoni katika Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrikondo (aliyevaa mtandio) akikabidhi mfano wa hundi kwa wanufaika wa tatu kutoka kulia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda

Akizungumza katika hafla ya utoaji fidia hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Mipango na Maendeleo Chuo Kikuu cha Sokoine Cha Kilimo SUA Dkt. Felix Nandonde amesema jumla ya wafidiwa 197 wamenufaika na malipo hayo.

Amesema SUA iliona kuna umuhimu wa kupanua shughuli zake kwa kuongeza maeneo baada ya kuanzisha Kampasi ya Mizengo Pinda Mkoani Katavi, Kampasi iliyoazishwa mwaka 2019 baada ya kupewa na Halmashauri ya wilaya ya Mpimbwe maeneo yenye ukubwa wa ekari 64 yenye majengo na ekari 200 zilizoko kitongoji cha Vilolo kilomita 8 kutoka chuoni.


Akizungumza katika hafla ya zoezi la kulipa fidia hiyo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda ameishukuru Serikali kwa kukubali kulipa fidia ili kuongeza eneo la Chuo hicho katika Kampasi ya Mizengo Pinda.

“Mimi nimefanya kazi Serikali Kuu kwa miaka 8 kabla ya kuja SUA, mara nyingi ukiwa kwenye kipindi cha uchaguzi na huu ndiyo mwezi wa uchaguzi, siyo rahisi kwa Serikali kutenga fedha kwa ajili ya kufanya tukio tunaloenda kulifanya leo, kwa hiyo tutambue kuwa huu ni muujiza ambao Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametutendea” amesema Prof. Chibunda

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanamvua Mrikondo amesema Serikali inayongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu ina nia ya dhati ya kuhakikisha inawahudumia wananchi katika nyanja zote ikiwemo elimu na kilimo.

Amesema Serikali imetoa kiasi hicho cha fedha ili kulipa wananchi na kuhakikisha Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kinakuwa na eneo la kutosha ili kuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi.

Katika hatua nyingine Mhe. Mrindoko amewataka wanufaika kuhakikisha fedha hizo zinawanufaisha wafaidika na hazivurugi amani katika familia zao bali ziwe chachu ya maendeleo huku akiwatahadharisha kuwepo kwa matapeli ambao hujitokeza mara tu mtu anapopata fedha.

Malipo hayo ya fidia ya mali, ardhi na kifuta machozi kwa makaburi 18 kinalipwa kwa wananchi 197 kutoka vitongoji vya Ndemanilwa, Kakuni na Lalanayo wanaoishi katika Halmashauri ya Mpimbwe ambao wanapisha upanuzi wa chuo kwenye eneo lenye ukubwa wa jumla ya ekari 690 sawa na hekta 279.







Post a Comment

0 Comments