Na: Farida Mkongwe
Rais na
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Simon Fraser (SFU) cha Canada, Dkt. Joy Johnson,
amesema ushirikiano wa Muungano wa vyuo vikuu vitano ni chachu muhimu ya
kukabiliana na changamoto kubwa za kidunia kama mabadiliko ya tabianchi na
maendeleo endelevu.
Dkt. Johnson amesema Kongamano la Pili la Kisayansi la Muungano huo ambalo limefanyika mjini Morogoro limekuwa jukwaa muhimu la kuwaleta pamoja watafiti na washiriki kutoka vyuo mbalimbali kujadili namna ya kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Amefafanua
kuwa, mbali na ushirikiano huo wa pamoja, vyuo hivyo pia vinaendesha miradi
mingine inayohusiana na kilimo na teknolojia sambamba na kutoa fursa za mafunzo
kwa wanafunzi.
“Kupitia mikutano inayoendelea kufanyika na Makamu Wakuu wa Vyuo vikuu mbalimbali, itabainisha maeneo mapya ya ushirikiano yatakayoongeza ufanisi wa programu hizo na kuleta tija katika sekta muhimu za maendeleo”, amesema Dkt. Johnson.
Dkt.
Johnson amesema moja ya maeneo mapya ya ushirikiano ni programu za mafunzo kwa
vitendo zinazowawezesha wanafunzi kujifunza moja kwa moja mashambani,
kushirikiana na wenzao na kupata maarifa kuhusu teknolojia mpya zinazoweza kusaidia
sekta ya kilimo, hatua inayolenga kuongeza ujuzi wa vitendo na kuimarisha uwezo
wa wanafunzi katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. William Anangisye, amesema Muungano huo ni ushahidi wa dhati wa matokeo chanya yanayoweza kupatikana pale taasisi zinaposhirikiana kuvuka mipaka na taaluma.
Amesema
mshikamano huu umeendeleza ubunifu, kujenga uwezo wa walimu na wanafunzi, na
kuchochea tafiti zenye mchango wa moja kwa moja katika jamii.
Akizungumza katika kongamano hilo, Prof. Anangisye ameishukuru SUA kwa maandalizi bora na mapokezi ya kipekee kwa washiriki, huku akimpongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, kwa mchango mkubwa wa wizara katika kuimarisha mfumo wa elimu ya juu nchini kupitia sera na uwekezaji wa kimkakati.
Kwa upande wake, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kupitia Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Raphael Chibunda, kimeendelea kutoa mchango mkubwa katika elimu ya kilimo, misitu, mazingira na wanyamapori.
Chuo
hicho kimekuwa mstari wa mbele kuhamasisha jamii kuhifadhi misitu na kuendeleza
tafiti za ugani zinazosaidia wakulima kuongeza uzalishaji bila kuharibu
mazingira.











0 Comments