Na: Farida Mkongwe
Mshikamano
wa kitaaluma, ubunifu na utafiti kati ya vyuo vikuu nchini umetambuliwa kuwa ni
nguzo muhimu ya matokeo chanya katika nyanja za elimu na kuboresha maisha ya
binadamu kwa kushughulikia changamoto zinazokabili jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Kongamano la Pili la Kisayansi la Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano, Prof. Japhet Kashaigili kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakati akizungumzia malengo ya kongamano hilo linalofanyika mjini Morogoro.
Prof.
Kashaigili amesema kongamano hilo limewakutanisha wataalamu na washiriki
takribani 200 kutoka vyuo vikuu vitano vya ndani na nje ya nchi, ikiwemo SUA,
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Aga Khan, Chuo Kikuu cha Nelson
Mandela, na Chuo Kikuu cha Simon Fraser cha Canada, ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa kitaaluma na utafiti yaliyofikiwa
na vyuo hivyo.
“Lengo la kongamano hili ambalo kwa mwaka huu
limeratibiwa na SUA ni kubadilishana uzoefu na wataalamu, kuimarisha uwezo wa
walimu na wanafunzi, pamoja na kuandaa machapisho ya pamoja ya tafiti
yatakayosaidia kutafuta suluhisho la changamoto za kijamii,” amesema
Prof. Kashaigili.
Aidha, amebainisha kuwa ubunifu unaozalishwa kupitia ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza tija ya kilimo, kuboresha huduma za afya na maji safi, sambamba na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kujadili kwa kina hatua za kitaaluma na kiteknolojia zinazoweza kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kongamano
hilo pia limekuwa fursa muhimu kwa watafiti chipukizi kuwasilisha tafiti zao na
kujenga mitandao ya kitaaluma, hatua ambayo itasaidia kuendeleza mashirikiano
haya kwa vitendo ili kuhakikisha tafiti zinazozalishwa zinakuwa na matokeo
chanya kwa taifa na dunia kwa ujumla.
Kongamano
la Pili la Kisayansi la Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano mwaka huu limebeba
kaulimbiu: “Zaidi ya Kuishi: Kujenga
Jamii Shirikishi na Zinazostahimili Mabadiliko ya Tabianchi.”






0 Comments