SUAMEDIA

Ugonjwa wa homa ya kiwele wapunguza mapato ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa

 Na: Ayoub Mwigune

Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa barani Afrika, hususan nchini Tanzania, wameendelea kukabiliwa na upungufu wa mapato kutokana na ugonjwa wa homa ya kiwele (mastitis) unaoathiri uzalishaji na ubora wa maziwa.

Ugonjwa huu umekuwa changamoto kubwa kwa wafugaji kutokana na gharama kubwa za matibabu pamoja na kupungua kwa ufanisi wa dawa zinazotumika kukabiliana nao.

Hayo yamebainishwa katika utafiti unaoendelea kufanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) chini ya uongozi wa Prof.  Gaymary Bakari, kupitia mradi unaolenga kuchunguza hali ya maambukizi ya homa ya kiwele na usugu wa vimelea vinavyosababisha ugonjwa huo dhidi ya dawa.

Kwa mujibu wa Prof. Gaymary, homa ya kiwele ni ugonjwa unaoathiri sehemu ya kiwele cha ng’ombe wa maziwa na husababishwa na vimelea, majeraha, uchafu au lishe duni ambapo athari zake  kubwa ni kupungua kwa uzalishaji wa maziwa, kushuka kwa ubora wake, na ongezeko la gharama za matibabu kwa wafugaji.

“Changamoto kubwa tuliyonayo sasa ni ongezeko la vimelea sugu kwa dawa zinazotumika mara kwa mara kama penicillin, oxytetracycline na sulphadimidine, hali hii inaongeza gharama za matibabu na kupunguza ufanisi wa tiba,” ameeleza Prof. Gaymary.

Mradi huo ujulikanao kama NANO COM unatekelezwa katika mikoa ya Tanga, Iringa, Mbeya, Njombe na Arusha, ambapo tafiti zinafanyika ili kubaini vyanzo vya maambukizi ya homa ya kiwele na kubuni tiba mbadala, salama na nafuu zitakazowanufaisha wafugaji wa ng’ombe wa maziwa nchini Tanzania.






Post a Comment

0 Comments