Na: Mwandishi wetu
Timu
ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ikiongozwa na Dkt.
Richard Samson imefanikiwa kuokoa mtoto wa tembo aliyenaswa na mtego kando ya
Mto Ruhidgi, katika Pori la Akiba la Kilombero, Wilaya ya Malinyi mkoani
Morogoro.
![]() |
| Moja kati ya Maafisa kutoka TAWA na Madaktari kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo wakimsaidia Tembo huyo mdogo. |
Mtoto huyo wa tembo alikuwa amenasa kwa siku mbili kwenye mtego uliotengenezwa kwa kamba ngumu na kujeruhiwa mguu wa mbele, hali iliyokuwa ikihatarisha maisha yake kwa kuwa hakuweza kutembea, kutafuta chakula wala maji.
Uokoaji
huo, uliofanyika tarehe 19 Septemba 2025, ulishirikisha wataalamu wa SUA na
Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), ambayo inasimamia Pori la Akiba la
Kilombero. Baada ya kamba kuondolewa na jeraha kushughulikiwa, mtoto wa tembo
alirudi katika afya njema na kuungana na familia yake ya asili, huku akiendelea
kufuatiliwa kwa karibu na maafisa wa uhifadhi.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na Sera ya
Taifa ya Wanyamapori ya 2007, kitendo hicho ni mfano wa utekelezaji wa
kivitendo wa vita dhidi ya ujangili na umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali,
taasisi za elimu na jamii katika kulinda rasilimali za wanyamapori.
“Uokoaji huu ni
mfano halisi wa jinsi elimu, ujuzi wa kitaaluma na ushirikiano kati ya taasisi
za Serikali na elimu ya juu unavyoweza kuokoa maisha ya wanyamapori na kudumisha
maliasili yetu”, amesema Dkt.
Samson.
Kwa
upande wake, TAWA imeahidi kuendelea kumlinda mtoto wa tembo huyo hadi
atakapoimarika kabisa akiwa na familia yake.
Tukio hili pia linaendana na mkataba wa kimataifa wa CITES (1973) unaolinda wanyamapori walioko hatarini, na linachangia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) hususan SDG 15 kuhusu kulinda mifumo ya ikolojia ya nchi kavu, SDG 13 kuhusu kupambana na mabadiliko ya tabianchi, na SDG 17 kuhusu kuimarisha ushirikiano ili kufikia malengo.

0 Comments