Na; Siwema Malibiche:
Chuo Kikuu
cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za elimu
ya juu nchini, kimezindua rasmi mradi wa miaka mitano wenye lengo la kuongeza
mnyororo wa thamani wa mazao ya mpunga na bustani, ikiwa ni sehemu ya mkakati
wa kuwawezesha vijana na wanawake kupata ajira bora na stadi za kujiajiri
katika sekta ya kilimo.
| Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Mipango, Utawala na Fedha Prof. Amandus Muhairwa akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mradi wa pili (kulia) ni Mratibu Mkuu wa Mradi, Dkt. Hamisi Tindwa |
Mradi huu unatekelezwa chini ya ufadhili wa shirika
la kimataifa lisilo la kiserikali la’Mastercard Foundation’ kupitia jukwaa la
vyuo vikuu vya kikanda (RUFORUM), na utatekelezwa kuanzia mwaka 2025 hadi
Desemba 2029.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo,
Mratibu Mkuu wa Mradi, Dkt. Hamisi Tindwa, amebainisha kuwa lengo kuu ni
kuwawezesha vijana kupata ujuzi kupitia mafunzo ya vitendo na nadharia katika
kilimo cha kisasa, ili kuunda ajira, kuongeza uzalishaji na kufikia soko lenye
tija.
![]() |
“Kupitia
mradi huu, zaidi vijana 1,000 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 wanatarajiwa
kunufaika kwa kupata ajira bora. Vilevile, wakulima zaidi ya 25,000 katika
maeneo ya utekelezaji wa mradi watafikiwa na kupewa mafunzo juu ya mbinu bora
za kilimo pamoja na njia za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,”
amesema Dkt. Tindwa.
Mradi huu
pia unalenga kuwajengea vijana uwezo wa kuajirika na kujiajiri katika sekta ya
kilimo, hasa katika mnyororo wa thamani wa mazao ya mpunga na bustani, huku
ukitilia mkazo matumizi ya teknolojia bunifu za kilimo na usindikaji.
Aidha, Rasi
wa Ndaki ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Kiongozi
Mshiriki wa Mradi, Dkt. Nyambilila Amuri,
ameeleza kuwa mradi huu ni fursa adhimu kwa vijana kushiriki kikamilifu
katika kupanua mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo kwani umelenga
kuwashawishi na kuwahamasisha wakulima kujiunga na kuwekeza katika kilimo kwa
kuwapatia mazingira rafiki, teknolojia bunifu na stadi muhimu zitakazowasaidia
kufanya kilimo chenye tija na chenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya taifa
![]() |
Kwa upande wake, Dkt. Leonard Binamungu, Mhadhiri
kutoka Idara ya Sayansi na Uhandisi wa Kompyuta, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa vijana katika mradi huo, akieleza kuwa
teknolojia ni nyenzo muhimu katika kuboresha kilimo na kuongeza tija.
“Sisi kama wataalamu wa teknolojia tuna mengi ya
kuwafundisha vijana. Kupitia mradi huu, vijana wataweza kujifunza namna ya
kubuni mifumo ya kidigitali itakayowawezesha wakulima kupata masoko kwa urahisi
na kwa ufanisi zaidi,” amesema Dkt. Binamungu.
![]() |
Mradi huu unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine
cha Kilimo (SUA) kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Arusha, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT). Moja ya
mikakati ya utekelezaji ni kuhuisha mitaala ya vyuo ili iendane na mahitaji ya
sasa ya soko na kuhimiza ubunifu wa teknolojia mpya za uzalishaji na kuongeza
thamani kwenye mazao.



0 Comments