SUAMEDIA

Prof. Nombo: Ushirikiano wa Vyuo Vikuu ni nguzo ya maarifa endelevu

 Na: Farida Mkongwe

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imesema ushirikiano wa Vyuo vikuu ni chanzo cha maarifa, ubunifu wa suluhisho na nguzo ya kulinda vizazi vijavyo kwa maendeleo endelevu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne  Nombo, wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Kisayansi wa Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano ambavyo ni Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika (NM-AIST) na Chuo Kikuu cha Simon Fraser (SFU), Canada uliofanyika Sept 30, 2025 mjini Morogoro.

Prof. Nombo amepongeza juhudi zinazofanywa na vyuo hivyo na kutolea mfano  wa kazi bora zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) katika kilimo endelevu ambazo zimewezesha jamii kukabiliana na mabadiliko ya mazingira.

Amesema mkutano huo ni muhimu sana kwa kuwa jamii zinakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, usalama wa chakula, mifumo dhaifu ya afya na ukosefu wa usawa wa kijamii.

“Mathalani, ukame wa hivi karibuni nchini Tanzania umepunguza mavuno kwa kiwango kikubwa na kuonesha haja ya kuimarisha kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, aidha janga la UVIKO-19 limetufundisha umuhimu wa kuwa na mifumo imara ya afya”,amesema Prof. Nombo.

Aidha, Prof. Nombo amesisitiza nafasi ya Muungano wa vyuo hivyo katika kushirikiana na kubadilishana rasilimali, vifaa vya utafiti na wataalamu na kwamba kupitia ushirikiano huo ubora wa tafiti unaweza kuongezeka, sera zikaimarishwa na majibu bunifu kupatikana kwa changamoto zinazokabili jamii za kikanda na kimataifa.

“Nachukua nafasi hii kukipongeza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na washirika wake kwa kuandaa jukwaa hili muhimu linalounganisha wasomi, watunga sera na wataalamu mbalimbali ili kutafuta suluhisho endelevu na shirikishi”, amesema  Prof. Nombo..

 Akitoa hotuba ya ukaribisho, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUA  Prof. Raphael Chibunda, amesema mkutano huo umelenga kuunganisha watafiti na wadau kushughulikia changamoto za dunia zinazohusu afya, usalama wa chakula, mazingira na tabianchi.

Prof. Chibunda amesema SUA ikiwa ni Taasisi mwenyeji, inajivunia kuwa nguzo ya jukwaa hilo la kubadilishana mitazamo, kuunda ushirikiano na kutafsiri utafiti kuwa vitendo.

Aidha, Prof. Chibunda amewahimiza washiriki kushirikiana, kubadilishana mawazo na kuunda mikakati ya kudumu kwa ajili ya jamii zinazokabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, kwa kufanya majadiliano yenye tija pamoja na matokeo yatakayoacha alama chanya kwa vizazi vijavyo.





Post a Comment

0 Comments